2014-01-20 12:15:09

Vita na kinzani za kijamii vinaangamiza maisha ya watoto wengi Barani Afrika


Baba Mtakatifu Francisko, hivi karibuni katika ujumbe wake kwa watumiaji wa mitandao ya kijamii alisema kwamba, vita inayoendelea sehemu mbali mbali za dunia inaangamiza maisha ya watoto wengi. Hawa ni watoto ambao wamepokonywa zawadi ya maisha ya utotoni.

Mustakabali wa watoto wengi Barani Afrika hasa katika Nchi kama Sudan ya Kusini, Jamhuri ya Afrika ya kati, DRC na kwingineko uko mashakani. Angalisho hili limetolewa hivi karibuni na Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa, UNICEF. Watoto ndio wanaoendelea kuathirika kwa kiasi kikubwa na vita inayoendelea huko Sudan ya Kusini. Inakadiriwa kwamba kuna zaidi ya watu 400, 000 hawana makazi maalum nchini humo na kuna idadi kubwa ya watu wanaendelea kufariki dunia.

Katika siku za hivi karibuni zaidi ya watu, 200, 000 wamekimbilia kwenye Kambi za Wakimbizi zinazosimamiwa na Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa. Mwakilishi wa UNICEF Barani Afrika Bwana Lyorlumun Uhaa anasema, kamwe watoto wasihusishwe kwenye mgogoro wa kivita na kama ikitokea hali kama hii vyama husika viwajibishwe kisheria.

Hivi karibuni watoto wenye umri kati ya miaka 14 hadi 17 waliokuwa wametekwa nyara na kikundi cha watu wenye silaha Mjini Bangui, Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, wameachiwa huru baada ya mazungumzo mazito kati ya Wawakilishi wa Umoja wa Mataifa na Serikali ya Mpito. Watoto hao kwa sasa wanahudumiwa kwenye Kambi zinazosimamiwa na Umoja wa Mataifa na wamepewa fursa ya kuendelea na masomo yao wakati ambapo mipango ya kuwarudisha kwenye familia zao inaendelea kufanyika.

Ukosefu wa ulinzi na usalama katika baadhi ya maeneo kunahatarisha maisha ya watoto wengi katika maeneo yenye vita na kinzani za kijamii, anasema Souleymane Diabatè, Mwakilishi wa UNICEF, Jamhuri ya watu wa Afrika ya Kati.







All the contents on this site are copyrighted ©.