Waratibu wakuu wa Utume wa Bahari, kitengo cha Baraza la Kipapa la wahamiaji na watu
wasiokuwa na makazi maalum, tangu tarehe 20 Januari hadi tarehe 24 Januari 2014 watakuwa
na mkutano mkuu unaowajumuisha wajumbe kutoka katika kanda tisa za Utume wa Bahari.
Hiki ni
kipindi cha kufanya tafakari ya kina sanjari na kushirikisha uzoefu na mang’amuzi,
tayari kuweka mikakati ya shughuli za kichungaji kwa Mabaharia na wavuvi sehemu mbali
mbali za dunia.
Kardinali Antonio Maria Vegliò katika hotuba yake ya ufunguzi
amewaambia wajumbe hao kwamba, watapata fursa ya kukutana na Baba Mtakatifu Francisko
hapo tarehe 22 Januari 2014 wakati wa Katekesi yake. Kanisa linatambua mchango mkubwa
unaoendelea kutolewa na Utume wa Bahari kama chombo cha Uinjilishaji, kinachotekeleza
utume na dhamana yake kwa njia ya safari, wongofu wa ndani na majiundo makini ya mtu
mzima: kiroho na kimwili. Utume wa Bahari unaongozwa na Mafundisho Jamii ya Kanisa.
Kardinali
Vegliò anahimiza umuhimu wa kujenga na kudumisha ari na moyo wa kiekumene katika ulimwengu
wa bahari, kwa kushirikiana na Wakristo kutoka katika Madhehebu mbali mbali; utume
ambao unapaswa kimsingi kuratibiwa na Idara za Utume wa Bahari kutoka katika Mabaraza
ya Maaskofu Katoliki pamoja na kushirikiana na Maaskofu mahalia.
Shughuli
za bahari zinazidi kuongezeka na kubadilika kwa haraka sana katika ulimwengu wa utandawazi
na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Wafanyabiashara wanataka kupata faida kubwa
kwa kubana matumizi na kuongeza tija na ufanisi. Wanachama wa Utume wa Bahari wanapaswa
kushirikiana na kushikamana kwa dhati, ili kutumia vyema rasilimali fedha na watu
iliyopo kwa kujenga na kukuza tija na weledi katika sekta ya biashara baharini lakini
kwa namna ya pekee katika kitengo cha uvuvi.
Utume wa Bahari anasema Kardinali
Vegliò unapaswa kuendelea kuhamasishwa kwa ari, bidii na uvumilivu mkubwa pengine
bado haujafahamika kwa wengi ndani ya Kanisa. Kipaumbele cha kwanza kiwe ni kwa ajili
ya wavuvi na familia zao. Hapa kuna haja ya kuweka mikakati ya kichungaji kwa ajili
ya kulisaidia kundi hili ambalo linaendelea kuteseka baharini, lakini lenye mafao
makubwa kwa maisha na uchumi wa kimataifa.
Kwa upande wake Askofu mkuu Joseph
Kalathiparambili, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la wahamiaji na watu wasiokuwa na
makazi maalum, amewatambulisha wawezeshaji wakuu katika mkutano huu. Kwavile mkutano
huu unafanyika katika Juma la kuombea Umoja wa Wakristo, hata wajumbe wa Utume wa
Bahari katika mkutano huu watashiriki kwa namna yao.
Wajumbe pamoja na mambo
mengine waanapembua kwa kina na mapana athari za utumwa mamboleo; dhuluma na nyanyaso
kwa mabaharia na wavuvi ambao mara kwa mara wanatekwa nyara baharini.