2014-01-20 09:53:37

Jubilee ya Miaka 150 ya Uinjilishaji endelevu Jimbo Katoliki Zanzibar


Jimbo Katoliki la Zanzibar, Jumapili tarehe 19 Januari 2014 limeadhimisha kilele cha Jubilee ya Miaka 150 ya Uinjilishaji endelevu Visiwani Zanzibar, kwa Ibada ya Misa Takatifu, iliyoongozwa na Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Idadi kubwa ya Maaskofu Katoliki Tanzania, Wawakilishi wa Makanisa na Dini mbali mbali kutoka ndani na nje ya Visiwa vya Zanzibar.

Ibada hii ya Misa Takatifu ilikuwa pia ni kilele cha kufunga Maadhimisho ya Mwaka wa Imani uliotangazwa na kuzinduliwa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI na kufungwa rasmi na Papa Francisko wakati wa Sherehe ya Kristo Mfalme wa Ulimwengu. Jimbo Katoliki la Zanzibar limesherehekea na kufunga rasmi Maadhimisho ya Siku kuu ya Utoto wa haki na amani.

Askofu Augustine Shao wa Jimbo Katoliki Zanzibar anabainisha kwamba, tangu mwanzo wa uwepo wake, Kanisa Katoliki limeendelea kuwa ni mdau mkubwa wa maendeleo endelevu ya wananchi wa Zanzibar katika ujumla wao. Limechangia kwa hali na mali katika sera na mikakati ya maboresho katika sekta ya elimu, afya na maendeleo ya umma. Hii ni dhana inayojionesha kwa Makanisa mengi yanayoendelea kutangaza Habari Njema ya Wokovu nchini Tanzania.

Askofu Shao anaendelea kueleza kwamba, tangu mwanzo wa Uinjilishaji, Kanisa lilitoa kipaumbele cha kwanza kwa mikakati ya elimu na afya, kama sehemu ya mchakato wa ukombozi wa mtu mzima: kiroho na kimwili. Mikakati hii inaendelea kufanyiwa kazi hata baada ya Miaka 50 ya Mapinduzi Zanzibar.

Kanisa bado linatoa huduma ya kutukuka katika sekta ya elimu na afya kama walivyofanya Wamissionari wa Shirika la Roho Mtakatifu walipofika kwa mara ya kwanza Visiwani Zanzibar, kunako mwaka 1863. Jimbo Katoliki la Zanzibar linaundwa na Parokia 8 zenye jumla ya Wakristo 11, 600. Kuna Parokia sita Kisiwani Unguja na Parokia mbili ziko Kisiwani Pemba.

Ukristo ulianza kuingia Zanzibar kunako Karne ya kumi na tano, juhudi hizi hazikuzaa matunda na Wamissionari wa Shirika la Roho Mtakatifu wakarudi tena Visiwani hapo kwa kasi na nguvu mpya, miaka 150 iliyopita, leo Jimbo Katoliki Zanzibar linaadhimisha Jubilee ya miaka 150 ya Uinjilishaji endelevu. Kardinali Polycarp Pengo katika mahubiri yake, amewataka waamini kulinda na kudumisha matunda ya kazi za Uinjilishaji endelevu yaliyopatikana katika kipindi cha Miaka 150 iliyopita hasa katika masuala ya imani, elimu na afya. Zanzibar ni lango la Imani ya Kikristo Afrika ya Mashariki.

Askofu Augustino Shao kwa upande wake anasema, watanzania kwa miaka mingi walikuwa na utamaduni wa kuheshimiana, kuvumiliana na kuthaminiana hata katika tofauti zao za kidini, kikabila na kiimani. Uvulimivu na mshikamano wa kitaifa unaanza kuyeyuka taratibu; lakini jambo la msingi kwa watanzania ni kukataa kugawanywa kwa misingi ya udini, ukabila na siasa.

Itakumbukwa kwamba, hivi karibuni Familia ya Mungu nchini Tanzania imeadhimisha Jubilee ya Miaka 150 ya Uinjilishaji nchini Tanzania sanjari na Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, uliofungwa mjini Bagamoyo, Jimbo Katoliki la Morogoro na kuhudhuriwa na umati mkubwa wa wawakilishi kutoka Majimbo yanayounda Kanisa Katoliki Tanzania.

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania. Linatarajia kufanya Hija ya Kitume mjini Vatican kuanzia tarehe 4 hadi tarehe 7 Aprili, 2014. Baraza la Maaskofu litapata fursa ya kuonana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko. Historia inaonesha kwamba, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kwa mara ya mwisho lilifanya Hija ya Kitume Mjini Vatican wakati wa uongozi wa Mwenyeheri Yohane Paulo II kunako mwaka 1987 na Mwaka 1996.

Mwezi Machi, 2005 Mwenyeheri Yohane Paulo II alikuwa amelazwa Hospitalini Gemelli, akabahatika kuonana na Kardinali Polycarp Pengo Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam pamoja na Askofu Severinus Niwemugizi aliyekuwa Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kwa wakati huo. Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili akawakabidhi ujumbe wake kwa Maandishi. Tarehe 2 Aprili 2004, Papa Yohane Paulo II akafariki dunia.

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania halikubahatika kufanya Hija ya Kitume Mjini Vatican wakati wa uongozi wa Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto VXI.








All the contents on this site are copyrighted ©.