2014-01-20 11:09:59

Bi Saada Mkuya Salum si mgeni sana kwa masuala ya fedha na uchumi!


Mabadiliko ya Baraza la Mawaziri Tanzania yaliyotangazwa na Rais Jakaya Kikwete kwa kumchagua Bi Saada Mkuya Salum kuwa Waziri wa Fedha ni kutaka kuendeleza sera ya fedha na uchumi wa Tanzania ambao kwa sasa unakua kwa kasi kubwa. Taarifa za Benki ya Dunia zinaonesha kwamba, uchumi wa Tanzania unatarajiwa kukua kwa asilimia 7 % ingawa bado Pato Ghafi la taifa liko chini ya asilimia 6. 2 kiwango kinachokubaliwa na Shirika la Fedha Kimataifa.

Bi Saada Mkuya Salum si mgeni sana kwa mambo ya fedha na uchumi, kwani itakumbukwa kwamba, tangu Mwaka 2012 alikuwa ni Naibu wa Wizara ya Fedha na kabla ya uteuzi huo alikuwa ni Kamishina wa Fedha kwenye Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Kwa bahati mbaya wataalam wa masuala ya kiuchumi wanasema, licha ya Tanzania kuwa na rasilimali na utajiri mkubwa wa maliasili, bado bajeti yake inategemea kwa kiasi kikubwa msaada kutoka katika nchi wafadhili. Hii ndiyo kazi itakayoendelezwa na Bi Saada Mkuya Salum katika wadhifa wake huu mpya kama alivyofanya hapo awali.

Wachunguzi wa masuala ya kiuchumi wanasubiri kuona ikiwa kama rasilimali kubwa inayoendelea kugunduliwa nchini Tanzania itatumika kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watanzania wengi au bado itaendelea kuwanufaisha wajanja wachache nchini Tanzania?







All the contents on this site are copyrighted ©.