2014-01-18 16:14:14

Zingatieni kanuni maadili kwa kuwaheshimu na kuwathamini watu ambao ndio walengwa wa matangazo ya Radio Na Luninga


Kampuni ya Televisheni ya Taifa nchini Italia, RAI imeadhimisha Miaka 90 tangu ilipoanza kurusha matangazo yake kwa njia ya radio na miaka 70 ya matangazo kwa njia ya Luninga kwa Ibada ya Misa Takatifu iliyoadhimishwa kwenye Ukumbi wa Paulo VI na kuongozwa na Kardinali angelo Comastri, Makamu Askofu, mjini Vatican. Ibada hii imehudhuriwa pia na wafanyakazi wa sekta ya mawasiliano kutoka nchini Italia kama kielelezo cha ushirikiano wa dhati kati ya RAI na Vatican katika huduma ya mawasiliano ya Jamii ndani na nje ya Italia.

Baba Mtakatifu Francisko ameipongeza taasisi hii kwa ushirikiano wa dhati katika masuala ya mawasiliano yanayomwezesha Khalifa wa Mtakatifu Petro kuwafikia wananchi wengi wa Italia na hata wale ambao wako nje ya Italia. Kuna ushirikiano mkubwa kati ya RAI, Radio Vatican na Kituo cha Televisheni cha Vatican, CTV. Kwa njia hii, RAI imeendelea kutoa huduma ya matangazo kwa hadhara na hivyo kuiwezesha kufuatilia matukio mbali mbali ndani na nje ya Italia.

Kati ya matukio yaliyotajwa na Baba Mtakatifu Francisko ni pamoja na: Maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, miaka hamsini iliyopita; uchaguzi wa viongozi wakuu wa Kanisa; maziko ya Mwenyeheri Yohane Paulo II bila kusahau Maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 2000 ya Ukristo pamoja na hija mbali mbali za kichungaji zinazofanywa na Khalifa wa Mtakatifu Petro nchini Italia.

Baba Mtakatifu anasema, miaka ya 1950 na 1960, kilikuwa ni kipindi cha maendeleo makubwa kwa RAI, kwani taasisi hii ilifanikiwa kurusha matangazo yake nchi nzima; ikajikita katika mafunzo ya wafanyakazi wake pamoja na kuboresha matangazo ambayo yanamgusa mtu mzima: kiroho na kimwili. Amegusia Sinema nyingi ambazo zimetengenezwa na RAI na kubaki kuwa na umaarufu wake katika historia. RAI imeshuhudia mabadiliko makubwa katika maisha na historia ya maisha ya wananchi wa Italia, kwa kusaidia mchakato wa ujenzi wa umoja wa kitaifa kwa njia ya lugha ya Kiitalia.

Baba Mtakatifu anawashukuru viongozi na wafanyakazi wa RAI na anawataka kujikita katika uwajibikaji mpana zaidi kwa siku za usoni, kwa kutambua kwamba, kazi yao ni kwa ajili ya huduma na mafao ya Jamii. Wafanyakazi wote wa RAI ni wadau muhimu sana katika mchakato wa elimu inayotoa habari, inayofurahisha na kuburudisha; inayofunda na kuwajibisha. Huu ni wajibu msingi unaopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza na wafanyakazi wote katika huduma za kijamii.

Baba Mtakatifu Francisko anakazia kanuni maadili katika mawasiliano ya jamii, kwa kuwaheshimu na kuwathamini watu, ambao kimsingi ni walengwa wa matangazo yanayotolewa na RAI. Kila mtu katika nafasi yake anawajibika kutoa kipaumbele cha kwanza kwa kanuni maadili. Baba Mtakatifu amewatakia kheri na baraka tele katika Kipindi cha Mwaka 2014. Anawataka wafanye kazi kwa bidii, juhudi na maarifa; daima wakiwa na imani na matumaini, ili kuweza kuionjesha Jamii ambayo ina kiu sana na tunu hizi msingi za maisha.







All the contents on this site are copyrighted ©.