2014-01-18 08:31:57

Warosmini kupata Mashemasi wawili mjini Roma


Askofu mstaafu Paolo de Nicolo, Jumapili tarehe 19 Januari 2014 anatarajiwa kutoa daraja takatifu la Ushemasi kwa Mafrateri wawili wa Shirika la Warosmini, kwenye Kanisa kuu la Giovanni Porta Latina, majira ya saa 10:00 Jioni kwa saa za Ulaya. Mashemasi wateule ni Fulgence Oisso na Richard Mwazia kutoka Jimbo Katoliki la Machakosi, Kenya. Ifuatayo ni historia fupi ya Frt. Fulgence Oisso. RealAudioMP3

Naitwa Frate Fulgence Oisso. Nimezaliwa katika Parokia ya Useri, Jimbo Katoliki la Moshi, Tanzania. Ninatoka katika Familia ya watoto saba na mimi nikiwa ni mtoto wa sita. Nililelewa katika misingi ya kikristo tangu nikiwa mdogo. Mama alipenda sana kunipeleka Kanisani na ndipo nilipotamani kuwa kasisi kabla hata sijaanza shule, pia Bibi mzaa mama alikuwa akitufundisha sala mbali mbali hasa sala za jioni, asubuhi na kabla ya kula na kisha kula. Wazazi walikuwa wakinihimiza kama ninataka kuwa Padre basi ni sharti niwe mtu wa sala na mtoto mwenye nidhamu na bidii ya kazi.
Wito.

Nilipofika darasa la nne nilijiunga na kikundi cha Mtakatifu Aloisi, kinachotoa huduma ya kutumikia Kanisani. Nilikuwa pia ni mwanachama wa Chama cha Wito, kitalu cha kulelea miito mbali mbali ndani ya kanisa. Hapa nilijifunza mambo mengi, kiasi cha kuwa na hamu ya kumtumikia Mungu Altareni kama Padre.

Nilipomaliza darasa la saba, nilijiunga na Seminari Ndogo ya Uru, inayoendeshwa na Shirika la Mitume wa Yesu, kwa kidato cha kwanza hadi cha nne. Nilipohitimu kidato cha nne nilitaka kujiunga na Umbwe Shule ya Sekondari ila moyo haukunisukuma sana kwenda huko kwani nilikuwa nimeomba kujiunga na Shirika la kazi ya Roho Mtakatifu (Holy Ghost Fathers) walinikubali na niliweza kumalizia masomo yangu ya kidato cha Tano na Sita katika Seminari ya Usa river Arusha, Jimbo kuu la Arusha.

Baada ya kidato cha sita nililiwafahamu Warosmini kupitia kwa mwanafunzi mwenzangu na niliandika barua ya maombi ila sikupata jibu mapema. Nilikuwa nimeomba kujiunga na mashirika mengine na walinikubali ila mwishoni Warosmini walinijibu. Nilienda kukaa nao kwa wiki moja na nilivutiwa na kazi na maisha yao kwa ujumla, baada ya kutembelea sehemu mbali mbali wanazofanya kazi.

Nilijiunga na Warosmini kunako mwaka 2003 kwa malezi huko Lushoto, Jimbo Katoliki la Tanga. Malezi yalichukua miaka mitatu: kama mpostulanti na mnovisi. Baada ya hapo nilianza masomo ya Falsafa nchini Kenya katika Chuo cha Waconsolata kwa miaka mitatu na baadaye nilitumwa nchini Italia kwa masomo ya taalimungu katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Laterani. Kwa sasa niko mwaka wa mwisho. Miaka hii ya malezi na majiundo ya Kipadre nimekuwa nikifanya mazoezi ya uchungaji sehemu mbali mbali kama, Hospitalini, kukaa na watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi, kutembelea wafungwa na wazee na pia kusaidiana Parokiani.

Mpaka sasa nafurahia maisha niliyochagua mwenyewe hasa katika Shirika la Warosmini na kuwa mrosmini baada ya kuweka Nadhiri za Daima mwaka 2012 na sasa namshukuru Mungu ninapokaribia kupokea Daraja Takatifu la ushemasi hapo tarehe 19 Januari 2014. Na yote yawezekana kwa sala na kuwa na matumaini. Napenda kuwashukuru wazazi na walezi wangu na wale wote walionisaidia kwa hali na mali mpaka nikafikia hatua hii. Mungu azidi kuwabariki na kuwajalia mema katika maisha na kazi zao.

Natambua kwamba, ushehasi ni huduma kwa Neno la Mungu, linalopaswa kutangazwa kwa njia ya ushuhuda wa maisha. Ni daraja la huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii, watu wanaopaswa kuonjeshwa Injili ya Furaha kwa njia ya matendo ya huruma na upendo. Shemasi ni mhudumu wa Sakramenti za Kanisa kadiri ya daraja hili ndani ya Kanisa: kwa kulisha na kuimarisha Imani ya Familia ya Mungu.

Shemasi anapaswa kuwa ni mtu wa sala na Ibada; anapaswa kuwa ni shahidi wa utakatifu wa maisha unaofumbatwa katika Mashauri ya Kiinjili. Ni matumaini yangu kwamba, mtaendelea kunisindikiza katika maisha na utume wangu kama Shemasi wa Shirika la Warosmini.








All the contents on this site are copyrighted ©.