2014-01-18 08:20:14

Tafakari ya neno la Mungu, Jumapili ya Pili ya Kipindi cha Mwaka wa A wa Kanisa


Mpendwa msikilizaji wa kipindi tafakari masomo Dominika, Dominika iliyopita tulimaliza kipindi na shamrashamra za Noeli na tulianza kipindi cha kawaida cha mwaka wa Kanisa. Ndiyo kusema sasa tunatafakari masomo Dominika ya II ya mwaka A. RealAudioMP3

Masomo Dominika hii: Somo la kwanza tunalipata katika Kitabu cha Isaya 49:3, 5-6. Somo II 1Kor. 1:1-3 na Injili Yn. 1:29-34 Mwaliko ni kutafakari na kuishi WITO WA KIKRISTO. Nabii Isaya yuko katika ndoto na anapokea wito wa Mungu kwa ajili ya taifa lake la Israeli. Isaya anaalikwa kutegemea nguvu za Mungu katika shughuli hiyo ya wito kwa ajili ya kuwarejeza watu wa Israeli katika amani na usalama. Mungu anamwahidia kuwa atakuwa nuru ya mataifa na hata miisho ya dunia. Tuko pia katika Juma la kuombea Umoja wa Wakristo, linaloongozwa na kauli mbiu ”Je, Kristo amegawanyika?”

Mpendwa mwana tafakari, ni vema na inafaa kujiuliza huyu mtumishi wa Mungu ni nani? Katika Agano la Kale tunakutana na sura ya mtumishi katika kitabu cha Nabii Yeremia 1:5 na hapa tunaona Mungu akimwambia Nabii Yeremia yakuwa alimteua tangu hajatungwa mimba na amemteua kuwa nabii kwa mataifa. Mwinjili Lk 1:15 anamtaja mtumishi ambaye hatakunywa divai wala kileo, na atajazwa Roho Mtakatifu tangu tumboni mwa mama yake. Fundisho hili linakuja wakati Waisraeli wako utumwani Babeli wanateseka na kwa njia ya nabii, Mungu anatangaza uhuru watakaoupata kwa njia ya mtumishi wa Mungu.

Kwa hakika aguo hili linakamilika katika Masiha, Yesu Mnazareti aliyezaliwa katika kipindi cha Noeli. Hawa manabii waliotangulia ambao walikuwa vyombo vyake wanatoa picha ya Masiha ambaye atatenda kadiri ya mpango wa Baba yake. Mpendwa msikilizaji kazi yako hivi leo pamoja na jumuiya na familia ni kuwa mtumishi mwaminifu kwa ajili ya kupeleka habari njema ya wokovu kwa mataifa.

Mtume Paulo akiwaandikia Wakorinto anawakumbusha juu ya wito wake na wito wa Sosthene na hasa ule wito mkuu wa kuwa watakatifu. Katika barua yake hiyo anaonesha kazi ya wito ikiwa ni kwa ajili ya kuwatakia wengine yaani taifa la Mungu mema yote ya mbinguni. Ndiyo kusema mpendwa msikilizaji wito ni kwa ajili ya kufariji na kushona mahali ambapo pamechanika katika harakati ya kuuendea uhuru kamili wa wana wa Mungu. Yafaa kukumbua kuwa wakati Paulo anawaandikia Wakorinto walikuwa katika ugomvi na ukosefu wa utulivu katika jumuiya yao. Akitangaza kwanza mamlaka aliyokabidhiwa na Kristo anawakemea na kuwambia nini maana ya kuwa mkristu. Kwa hakika ni kutumikia kwa furaha na kutenda kadiri ya matakwa ya Injili. Umoja kamili unajikita katika mafundisho ya Kristo ndiyo msingi wa maisha ya wito wetu.

Katika Injili nabii Yohane Mbatizaji anakiri ukuu wa Masiha akisema yeye ndiye aliyenipeleka na hivi ni kabla yangu na kabla ya yote. Ndiyo kusema Yohane Mbatizaji yuko tayari kushuka kwa maana wito ni ule wa kuonesha kwa mataifa yakwamba Kristu ni Mwanakondoo wa Mungu aondoaye dhambi za ulimwengu. Kwa hakika ile sifa yakwamba nilikuchagua kabla ya kutunga mimba haimwangukii Masiha kama wale manabii wa Agano la Kale, ndiyo maana basi Yohane anamtambulisha kama Mwanakondoo wa Mungu, ambaye utume wake ni kuondoa dhambi za dunia, dhambi zetu sote.

Kwa kutumia Mwanakondoo wa Mungu, anataka kuturudisha nyuma kutafakari ule usiku mtakatifu Waisraeli walipotoka Misri. Tunakumbuka kila familia ilichinja mwanakondoo na ilitumia damu kupaka milango na ikawa ni alama kwa wokovu wao. Ni kwa mantiki hiyo basi Yohane mwinjili anaweka mbele yetu Yesu atakaye toa maisha yake kwa njia ya kumwaga damu yake takatifu. Mtumishi huyu atateswa lakini kwa njia ya mateso yake atauokoa ulimwengu.

Mpendwa msikilizaji Yohane Mbatizaji analo jambo la kutuambia yakwamba hakumfahamu Masiha, hii ni hatua nzuri ambayo hivi leo wakatekumeni wanaanza nayo. Hawajui chochote lakini Mungu huwaita na polepole humtambua Bwana. Kama ambavyo nabii alibadilisha mwono wake kwa Masiha ndivyo ambavyo mkatekumeni anavyoalikwa kusafiri polepole katika njia ya utambuzi mpaka kilima kitakatifu. Mpendwa msikilizaji, twaweza kuzama katika ukatekumeni na kusahau kwamba hata sisi tunao wajibu wa kuendelea kutafuta maana ya wito wetu na hasa kutambua Masiha wetu si yule mfalme mkandamizaji bali mwenye huruma na hasa akiwatumikia wengine. Ndiyo kusema wito wetu tukimfuata yeye ni kuwa watumishi waaminifu wa Injili yake.

Mtazame Yohane Mbatizaji anakiri yakwamba, yeye mwenyewe hakumfahamu na ndiyo maana alitumwa akamshuhudie mbele ya mataifa kabla na katika udogo wake huo alitumwa akawabatize watu kwa maji ili kujiandaa kumpokea Masiha. Tena zaidi ya hilo anasema anapokuja habatizi kwa maji bali kwa moto na Roho Mtakatifu. Hii ni alama ya Masiha alama ambayo yamtofautisha toka Yohane Mbatizaji. Huyu kadiri ya Yohane Mbatizaji ni Mwana wa Mungu. Basi kukiri kwa nabii kutusaidie kuwa wanyenyekevu katika maisha yetu na hapo itakuwa rahisi kuhubiri habari njema.

Nikutakie furaha na amani katika kuwa mtumishi wa Mungu na hivi kuwa chombo cha mapatano na wokovu. Tumsifu Yesu Kristo.

Tafakari hii imeletwa kwako na Padre Richard Tiganya C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.