2014-01-18 16:40:26

Serikali ya Tanzania yatuma salam za rambi rambi kutokana na kifo cha Dr. Seydna M. Burhanuddin wa Jumuiya ya Dawoodi Bohra


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete ametuma salamu za rambirambi kwa Jumuia ya Dawoodi Bohra katika Tanzania kufuatia kifo cha Kiongozi wa Kiroho wa Jumuia hiyo duniani, Dkt. Seydna Mohammed Burhanuddin ambaye amefariki dunia asubuhi ya Ijumaa, Januari 17, 2014.

Dkt. Seydna Mohammed Burhanuddin, Kiongozi wa Jumuia ya Dawoodi Bohra kwa miaka 39 iliyopita, amefariki dunia nyumbani kwake katika kasri ya Saifee Mahal, eneo la Mahabar, kusini mwa jiji la Mumbai, India, kwa ugonjwa wa moyo akiwa na umri wa miaka 102. Katika salamu zake kwa Mwenyekiti wa Jumuia ya Dawoodi Bohra katika Tanzania, Sheikh Tayabali Sheikh Hamzabhai Patanwalla, Rais Kikwete amesema: “Nimepokea kwa huzuni na masikitiko taarifa za kifo cha Dkt. Seydna Mohammed Burhanuddin, Kiongozi wa Kiroho wa Jumuia ya Dawoodi Bohra duniani kwa miaka mingi ambacho nimejulishwa kimetokea subuhi ya leo nyumbani kwake mjini Mumbai, India.”

Rais kikwete amesema: “Seydna Mohammed Burhanuddin alikuwa kiongozi mwenye busara na kiongozi bora wa kiroho ambaye katika maisha yake yote alilenga siyo kutoa uongozi wa kiroho kwa Jumuia yake ya Dawoodi Bohra bali kuunganisha madhehebu na dini nyingine duniani kwa nia ya kuhakikisha kuwa waumini wa dini mbali mbali wanaishi kwa amani na upendo, na kwa kuvumiliana hapa duniani.”

“Nilimjua binafsi Dkt. Seydna Mohammed Burhanuddin na mara ya mwisho alipotembelea Tanzania nilipata nafasi ya kukutana na kuzungumza naye ambako nilizidi kujiridhisha kuwa huyu alikuwa ni kiongozi mwenye sifa za ziada siyo tu katika uongozi wa kidini lakini pia katika uongozi wa kijamii.”

Amesema Rais Kikwete: “Nakutumia wewe Mwenyekiti wa Jumuia ya Dawoodi Bohra nchini Sheikh Tayabali Sheikh Hamzabhai Patanwalla salamu zangu za rambirambi kuomboleza kifo cha Mzee wetu huyu. Na kupitia kwako, naomba unifikishie salamu zangu kwa wana-Jumuia nzima ya Dawoodi Bohra hapa nchini kwetu na popote duniani. Wajulishe kuwa naungana nao katika msiba huu mkubwa. Aidha, naungana nao katika kumwomba Mwenyeji Mungu, Mwingi wa Rehema, aiweke peponi roho ya Marehemu Seydna Mohammed Burhanuddin. Amina.”








All the contents on this site are copyrighted ©.