2014-01-18 08:57:04

Mshikamano wa kidugu na kiimani na wananchi wanaoishi Nchi Takatifu


Maaskofu kutoka Ulaya, Marekani na Afrika ya Kusini, hivi karibuni wamehitimisha hija ya kiroho Nchi Takatifu, kama kielelezo cha mshikamano wa imani na mapendo kwa wananchi wanaoishi katika Nchi Takatifu pamoja na kuwatia moyo Wakristo wanaoendelea kuteseka na kunyanyasika kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake.

Mshikamano huu ulianzishwa kunako Mwaka 1998 na kila mwaka kuanzia tarehe 11 hadi tarehe 16 Januari, Maaskofu wanafanya hija ya kiroho katika Nchi Takatifu. Maaskofu wanasema, Waisraeli na Wapalestina wana kiu na njaa ya kuona kuwa haki, amani na utulivu vinatawala tena katika mipaka ya nchi zao.

Maaskofu wanawataka viongozi wa Israeli na Palestina kuonesha utashi wa kisiasa kwa kuwajengea wanachi wao matumaini na kwamba, pasiwepo na mtu ambaye atakuwa ni kikwazo cha majadiliano ya amani na utulivu!

Maaskofu wanasema, wameridhishwa na uwepo wa Jumuiya za Kikristo hata katika udogo wake huko Nchi Takatifu. Wanaendelea kuwatia moyo na ari ya kusonga mbele pasi na kukata tamaa na kwamba, wakristo sehemu mbali mbali za dunia wataendelea kuwaunga mkono katika mchakato wa maendeleo endelevu kwa kuwasaidia katika kugharimia sekta ya elimu na mapambano dhidi ya umaskini. Hizi ni juhudi zinazowalenga wananchi wote wanaoishi katika Nchi Takatifu bila ubaguzi wa kidini.

Maaskofu wanawaalika Wakristo katika Nchi Takatifu kuendelea kutolea ushuhuda katika imani, matumaini na mapendo na kwamba, mapendo ya dhati ni chemchemi ya matumaini mapya kwa wale waliokata tamaa. Ni matumaini haya yanayowasukuma wadau mbali mbali kuendelea kuunga mkono mchakato wa majadiliano ya amani, ili kweli amani ya kudumu iweze kupatikana na kudumishwa katika Nchi Takatifu.

Hii ni amani inayopaswa kujikita katika haki na usawa kati ya Waisraeli na Wapalestina. Ukanda wa Ghaza ni kashfa na ukosefu wa haki msingi za binadamu; jambo linalohitaji kupatiwa ufumbuzi na Jumuiya ya Kimataifa. Maaskofu wanawaomba wanasiasa na wapenda amani duniani kusaidia maboresho ya maisha katika Ukanda wa Ghaza, ili watu waweze kupata mahitaji yao msingi kwa gharama nafuu.

Maaskofu wanaonesha matumaini makubwa kwa Hija ya Sala itakayofanywa na Baba Mtakatifu Francisko katika Nchi Takatifu, mwezi Mei, mwaka huu. Itakuwa ni fursa ya kuimarisha imani na matumaini katika Nchi Takatifu. Wanaamini kwamba, amani ya kudumu ni jambo linalowezekana kabisa.








All the contents on this site are copyrighted ©.