Kanisa linapenda kusimama kidete kulinda na kutetea haki za watoto!
Kanisa Katoliki linapenda kuwa mstari wa mbele na mfano wa kuigwa katika kulinda na
kutetea haki msingi za watoto sehemu mbali mbali za dunia, dhidi ya nyanyaso na mambo
yanayokwamisha malezi na majiundo ya watoto: kiroho na kimwili.
Hivi ndivyo
alivyobainisha Askofu mkuu Silvano Maria Tomasi, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican,
kwenye Ofisi za Umoja wa Mataifa zilizoko mjini Geneva wakati alipokuwa anawasilisha
taarifa ya utekelezaji wa haki za watoto kutoka Vatican kwenye mkutano wa sitini na
tano wa Umoja wa Mataifa kuhusu utekelezaji wa itifaki ya ulinzi wa haki za watoto
huko mjini Geneva, hapo tarehe 16 Januari 2014.
Askofu mkuu Silvano Maria Tomasi
anasema, Vatican imejibu maswali yote yaliyoulizwa na Umoja wa Mataifa kwa njia ya
maandishi kwa kufafanua sera na mikakati inayotekelezwa na Kanisa Katoliki katika
kukabiliana na nyanyaso na dhuluma dhidi ya watoto wadogo. Vatican imekwisha toa kanuni
elekezi kwa Makanisa mahalia jinsi ya kupambana na tabia hii chafu hasa katika taasisi
zake za elimu na majiundo.
Askofu mkuu Tomasi amebainisha kwa kina na mapana,
mikakati, sheria, kanuni na taratibu ambazo zimechukuliwa na Vatican kama sehemu ya
mchakato wa kupambana na nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo, kashfa ambayo
ililichafua Kanisa katika miaka ya hivi karibuni. Hizi ni juhudi ambazo zimevaliwa
njuga kwa namna ya pekee na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI pamoja na Papa Francisko
ambaye hivi karibuni aliunda Tume ya Kipapa ya Kulinda Watoto.
Askofu mkuu
Tomasi anasema, hakuna sababu yoyote ile inayoweza kuhalalisha nyanyaso dhidi ya watoto
wadogo, ndiyo maana Vatican inataka kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima
ya watoto wadogo katika hatua mbali mbali za malezi na makuzi yao; yaani tangu pale
mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake.
Jumuiya ya Kimataifa haina
budi kusimama kidete kulinda na kutetea pia haki msingi za familia; kitovu cha malezi
na makuzi ya mtoto. Wazazi wana haki na dhamana ya kutoa malezi na majiundo makini
kwa watoto wao pamoja na kuheshimu uhuru wa kidini. Hizi ni haki msingi za familia
katika malezi na makuzi ya watoto sehemu mbali mbali za dunia.
Ujumbe wa Vatican
unasubiri kwa hamu kusikia ushauri utakaotolewa na Umoja wa Mataifa kuhusiana na jitiahada
zake katika kulinda na kutetea utu na heshima ya watoto wadogo na kwamba, iko tayari
kuufanyia kazi ushauri huu, mintarafu malengo ya itifaki ya kulinda watoto iliyoridhiwa
na Jumuiya ya Kimataifa kunako Mwaka 1992.