2014-01-18 11:21:42

Diplomasia haina budi kujikita katika utu na heshima ya binadamu!


Kardinali mteule Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican katika mahojiano maalum na Kituo cha Televisheni cha Vatican, CTV anasema kwamba, sera ya kidiplomasia na ushirikiano wa kimataifa inayotekelezwa na Vatican inajikita katika kujali, kuthamini, kulinda na kudumisha utu na heshima ya binadamu. Mwanadamu na mahitaji yake msingi: kiroho na kimwili yanapaswa kushughulikiwa kikamilifu katika sera na mikakati ya maendeleo endelevu.

Hii ni changamoto ya kujenga na kudumisha mshikamano wa upendo unaongozwa na kanuni auni hasa katika ulimwengu huu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia ambako: vita, kinzani, migogoro, njaa na magonjwa yanaonekana kuwa ni mambo ya kawaida kabisa katika maisha ya mwanadamu. Katika hali kama hii inayoonesha kinzani, kuna haja kwa binadamu kupewa kipaumbele cha kwanza.

Kardinali mteule Parolin anasema, huduma ya Kidiplomasia inayotolewa na Vatican ni nyeti, yenye madai makubwa na uwajibikaji makini kwa namna ya pekee katika uongozi wa Baba Mtakatifu Francisko ambaye kwa sasa anafungua ukurasa mpya wa maisha na utume wa Kanisa. Changamoto na kipaumbele cha pekee kwa wakati huu ni kuhakikisha kwamba, Kanisa linatoka kifua mbele kutangaza Injili ya Furaha kwa kujikita katika dhana ya Kanisa ambalo ni la Kimissionari kwani kila Mkristo anaalikwa kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa njia ya ushuhuda wa maisha yake.

Kardinali mteule Parolin anasema kwamba, diplomasia ya Baba Mtakatifu Francisko inajikita kwa namna ya pekee katika kanuni maadili inayosimikwa katika mshikamano wa kidugu kwa ajili ya mafao ya wengi, jambo ambalo wengine wanadhani kwamba, ni ndoto ya kufikirika katika ulimwengu ambao umesheheni ubinafsi na uchu wa mali na madaraka.

Mara kwa mara Baba Mtakatifu ametoa mwaliko kwa ajili ya ujenzi na udumifu wa misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano, lakini pengine inaonekana kana kwamba, kilio hiki cha Baba Mtakatifu hakina tena msikilizaji. Ukweli wa mambo ni kwamba, watu wana kiu na njaa ya haki, amani, upendo na mshikamano ambao kimsingi ni kikolezo cha maendeleo endelevu yanayozingatia mahitaji msingi ya binadamu wote. Kuna mikakati inayoendelea kufanywa na Jumuiya ya Kimataifa katika ujenzi wa haki na amani sehemu mbali mbali za dunia.

Kardinali mteule Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anaendelea kufafanua kwamba, diplomasia na mikakati ya ushirikiano wa kimataifa haina budi kutoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu na mahitaji yake msingi. Huu ndio mkakati unaofanyiwa kazi na Baba Mtakatifu Francisko kwa nyakati hizi. Mwanadamu apewe umuhimu unaostahili kwa kujenga na kudumisha pia mshikamano wa dhati na maskini pamoja na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na hali yao ya maisha.

Watu wajenge na kudumisha utamaduni wa kukutana ili kuondokana na ubinafsi unaowafanya watu wengi kuishi kana kwamba, wako kisiwani bila ya kuwa na mahusiano ya kidugu na jirani zao. Mshikamano wa kidugu unapania kudumisha utamaduni unaojali na kuguswa na mahitaji ya jirani. Watu wasiridhike na idadi, bali watambue kwamba, kila mtu mmoja mmoja anathamani kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu.

Ndiyo maana hata wakati Baba Mtakatifu anapokutana na makundi makubwa ya watu, lakini hata katika makundi haya, bado kuna watu anawaita kwa majina kuonesha kwamba, anawatambua na kuwajali. Kwa maneno mengine, anasema Kardinali mteule Parolin, mahusiano ya kidiplomasia hayana budi kusimikwa katika fadhila ya upendo; majadiliano ya kina yanayosimikwa katika ukweli na uwazi; kuna haja ya kuheshimiana na kujaliana hata katika tofauti msingi za kibinadamu.

Kamwe tofauti hizi zisiwe ni chanzo cha vita, vurugu na kinzani za kisiasa, kijamii, kiuchumi na kikabila, bali utajiri unaopania kujenga na kudumisha mafao ya wengi. Huu ndio mwelekeo sahihi wa diplomasia inayopigiwa debe na Vaticani







All the contents on this site are copyrighted ©.