2014-01-18 09:07:02

Athari za mafuriko Mkoani Dodoma


Waziri mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda ametembelea vijiji vya Chipogoro na Fufu katika wilaya za Mpwapwa na Chamwino, mkoani Dodoma na kukagua maeneo mbalimbali ambayo yaliathiriwa na mafuriko kutokana na mvua kubwa zilizonyesha kati ya Januari 2 hadi Januari 11, mwaka huu.

Akiwa katika kijiji cha Chipogoro tarafa ya Rubi, Waziri Mkuu alikagua kituo cha polisi na nyumba zilizobomolewa, choo cha zahanati na kukagua eneo la barabara inayojengwa ya kutoka Dodoma hadi Iringa katika eneo lenye matatizo ya makaravati kuziba.

Kwenye kijiji cha Fufu katika tarafa ya Makangwa ambacho kiko umbali wa kilometa 30 kutoka Chipogoro, Waziri Mkuu alikagua maeneo ya makazi yaliyoathiriwa kwa mafuriko na kukagua baadhi ya nyumba zilizobomoka kabla ya kuzungumza na wananchi na kuwapa pole.

Akizungumza na wakazi wa vijiji hivyo Ijumaa, Januari 17, 2014), mara baada ya kupokea taarifa za maafa ya mafuriko hayo, Waziri Mkuu alimtaka Meneja wa TANROADS mkoa wa Dodoma, Eng. Leonard Chimagu kuhakikisha anasimamia wakandarasi wa barabara hiyo ambayo ujenzi wake bado haujakamilika na kuainisha maeneo korofi ili yafanyiwe marekebisho haraka.

“Nimekagua matundu katika daraja moja pale Chipogoro na kuona ni madogo, mtaalamu anasema uchafu ulioziba ndiyo umesababisha maji yasipite. Mimi si mhandisi na hizi ni mvua za kwanza tu, sasa yakija maji mengi zaidi ya haya hali itakuwaje?, alihoji Waziri Mkuu.

“Hata hapa Fufu, kuna mahali nimeona maji yanaonyesha yalikuja kwa kasi kubwa lakini upenyo wa kuingia kwenye makaravati na kutokea upande wa pili ni mdogo sana... barabara hii ni mkombozi lakini kama haitazingatia uhalisia wa maeneo itakuwa ni balaa,” alionya.

Alimtaka pia awasimamie wakandarasi hao ili wanapoweka matoleo ya maji wahakikishe upande wa pili barabara maji hayo yanakwenda kwenye mikondo ya mto na siyo kuyaacha tu yasambae kiholela na kuishia kwenye makazi ya watu au mashamba yao.

Waziri Mkuu aliahidi kutoa mifuko ya saruji 2,600 na mabati 1,560 ambapo kila kijiji kitapata mifuko 1,300 na mabati 780 ili kuwasaidia wakazi waliobomolewa nyumba zao waweze kujenga nyumba za kisasa.

Alimwagiza Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Rehema Nchimbi kuwashirikisha wadau wengine katika mkoa huo ili waone wanawezaje kuchangia upatikanaji wa mabati mengi zaidi kwa ajili ya nyumba zilizoezuliwa.

Kuhusu chakula cha msaada, Waziri Mkuu alimtaka Dk. Nchimbi aandae makisio ya mahitaji ya chakula yaliyopo na kuyafikisha Ofisi ya Waziri Mkuu ambako kuna Idara inayosimamia maafa ili waletewe chakula hicho haraka kwa sababu kipo.

Alisema anakubaliana na ushauri uliotolewa kuhusu suala la ujenzi wa mabwawa ya kukinga maji ya mvua ili kupunguza kasi ya maji yanayoporomoka kutoka milimani lakini akasema Serikali imeanza na ujenzi wa Bwawa la Kidete lililoko wilayani Kilosa tangu yaliyopotokea mafuriko wilayani humo.

Mapema, akitoa taarifa kwa Waziri Mkuu, Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Bw. Alfred Msovella, alisema nyumba 129 zilibomoka, vyoo 78 vimebomoka kikiwemo cha zahanati ambapo wakazi 1,390 wamepoteza vifaa mbalimbali ikiwemo vyakula, magodoro, vyombo vya ndani na mifugo.

Bw. Msovella ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Kongwa alisema hivi sasa, wakazi hao wanahitaji mahema 400, magodoro 381, madaftari ya wanafunzi na dawa za matibabu.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Bi. Fatma Salum Ally akitoa taarifa mbele ya Waziri Mkuu kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa shule ya msingi Fufu, alisema jumla ya nyumba 26 zilibomolewa na mali kama vyakula, samani, vyombo vya nyumbani na bidhaa za biashara kuharibika.

Alisema eneo la kijiji cha Fufu ni tambarare na liko chini ya safu za milima na maji ya mvua yanayoporoka kutoka milimani, huondoka polepole. “Hata hivyo, hali hii ya mafuriko imechochewa na ujenzi wa barabara kuu kwa kiwango cha lami ambapo tuta la barabara mpya na vidaraja vidogo vilivyowekwa vimekuwa kizuizi cha maji mengi yanayotoka milimani na hivyo kuongeza tatizo la mafuriko,” alisema.

Mikutano hiyo ilihudhuriwa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Bw. Gregory Teu ambaye pia ni mbunge wa Mpwapwa pamoja na mbunge wa Mtera, Bw. Livingstone Lusinde.








All the contents on this site are copyrighted ©.