2014-01-17 14:13:05

Wakristo msikumbatie malimwengu na kulitema neno la Mungu


Wakristo watambue kwamba, zawadi ya kuwa ni Watoto wa Mungu inawawajibisha kulisoma, kulitafakari na kulimwilisha Neno la Mungu katika maisha yao na wala si kufanya vinginevyo kana kwamba, hakuna Mwenyezi Mungu; kwa kutenda kadiri ya matakwa yao binafsi pamoja na kukumbatia malimwengu.

Haya ndiyo yaliyowatokea Waisrael katika Agano la Kale kwa kumkataa Mwenyezi Mungu na kutaka kukumbatia malimwengu kwa kuiga mtindo wa maisha kutoka kwa nchi jirani. Waisraeli walimkataa Nabii Samueli wakadhani wanamkataa yeye tu, lakini Mwenyezi Mungu aliwakumbusha kwamba, walikuwa wanamkataa hata Yeye ambaye ndiye Mungu wao.

Baba Mtakatifu katika mahubiri yake Ijumaa, tarehe 17 Januari 2014 kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha anasema kwamba, Wazee wa Waisraeli, walikuwa wanatema upendo, huruma na ukarimu kutoka kwa Mwenyezi Mungu; uliomsukuma hata akawateuwa kuwa ni Taifa takatifu na wateule wa Mungu. Hii ni changamoto kwa Wakristo kuwa waaminifu kwa Mwenyezi Mungu na kamwe wasikubali kishawishi cha kumkana na kutaka kuyakumbatia malimwengu.

Wakristo waendelee kujishikamanisha na Mwenyezi Mungu kwa kufuata sheria na amri zake. Neno la Mungu liwe ni dira na mwongozo wa maisha ya Mkristo, kamwe wasijisie wanyonge mbele ya watu wa mataifa! Wao ni wana wateule wa Mwenyezi Mungu, kumbe wanapaswa kutoka kifua mbele kushuhudia imani hii kwa njia ya matendo adili. Walegeze mioyo yao, tayari kulipokea na kulimwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha.

Wakristo wajitahidi kuiga mfano wa Bikira Maria aliyekuwa Tabernakulo ya kwanza ya Neno la Mungu, aliyefanyika Mwili, Mama aliyethubutu kuhifadhi na kulitafakari Neno la Mungu katika hija ya maisha yake hapa duniani. Waamini waoneshe unyenyekevu katika maisha ya kiroho, tayari kupokea neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu.








All the contents on this site are copyrighted ©.