2014-01-17 14:21:44

Umoja na mshikamano wa kikristo ujioneshe katika majadiliano ya kiekumene kiroho kwa kujikita katika amri ya upendo kwa Mungu na jirani!


Katika kipindi cha miaka 25 iliyopita, Mwenyeheri Yohane Paulo II, Papa mstaafu Benedikto XVI na sasa Baba Mtakatifu Francisko, wamekuwa wakikutana na kuzungumza na Ujumbe wa Kiekumene kutoka Finland, katika Maadhimisho ya Mtakatifu Enric, Msimamizi wa Finland. Huu ni ushuhuda katika mchakato wa kutafuta umoja kamili miongoni mwa wafuasi wa Kristo. Juma la kuombea umoja wa Wakristo kwa Mwaka 2014 linaongozwa na kauli mbiu “Je, Kristo amegawanyika?”

Hili bado ni swali msingi ambalo Mtakatifu Paulo anaendelea kuwauliza Wakristo katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo. Changamoto kubwa iliyoko mbele ya Wakristo ni kujenga umoja kamili miongoni mwa Wakristo kama alivyosali Kristo mwenyewe akiwaombea kwa Baba yake wa mbinguni ili wote wawe wamoja!

Ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa, tarehe 17 Januari 2014 wakati alipokutana na kuzungumza na ujumbe wa Kiekumene kutoka Finland unaofanya hija ya kiekumene mjini Roma. Kumekuwepo na maendeleo makubwa katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene ndani ya Makanisa, kwani wanachangamotishwa kushuhudia imani yao kati ya watu wanaowazunguka, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa uwepo wa Mwenyezi Mungu. Tatizo la ukanimungu ni kubwa si tu Barani Ulaya, bali limeenea sehemu mbali mbali za dunia.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, ushuhuda wa wakristo unapaswa kujisimika zaidi katika imani, kwa kumwilisha upendo wa Mungu uliofunuliwa kwa njia ya Yesu Kristo, Mwanaye Mpendwa. Umoja na mshikamano wa Kikristo, ujioneshe katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene kiroho, yanayojikita katika amri ya upendo kwa Mungu na jirani; wongofu wa ndani, utakatifu na maisha ya sala.

Baba Mtakatifu anasema, majadiliano ya kiekumene ni mchakato wa maisha ya kiroho unaotekelezwa kwa kuwa waaminifu katika utekelezaji wa mapenzi ya Mwenyezi Mungu, chini ya usimamizi wa Roho Mtakatifu. Ni mwaliko wa kuendelea kusali bila kuchoka kwa kumwomba Roho Mtakatifu awaongoze katika ukweli mkamilifu, ili hatimaye, Wakristo waweze kuwa ni vyombo vya upatanisho na umoja.








All the contents on this site are copyrighted ©.