2014-01-16 09:12:38

Watanzania wanaomboleza kifo cha Jaji George Liundi, Msajili wa kwanza wa Vyama vya Siasa Tanzania


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amesikitishwa na kuhuzunishwa na kifo cha ghafla cha aliyekuwa msajili wa kwanza wa vyama vya siasa nchini, Jaji George Liundi kilichototokea Januari 12, 2014, nyumbani kwake Keko, mjini Dar Es Salaam.

Katika salamu zake za rambirambi ambazo alizituma kwa Msajili wa Vyama vya Siasa nchini Jaji Francis Mutungi, Rais Kikwete amesema kuwa amepokea taarifa cha kifo cha Bwana Liundi kwa masikitiko na huzuni. “Bwana Liundi alikuwa mtumishi mtiifu wa umma, alikuwa mchapakazi wa kuaminika na alikuwa mwandishi hodari wa sheria. Tutamkumbuka kama mtumishi mwadilifu na mwaminifu wa umma na mfano wa kuigwa wa utumishi bora,” amesema Rais Kikwete katika salamu zake za rambirambi na kuongeza:

“Nakutumia wewe Msajili wa Vyama vya Siasa Tanzania Jaji Francis Mutungi salamu zangu za rambirambi, nikiungana nawe kuomboleza kifo cha Bwana Liundi. Aidha, kupitia kwako nawatumia wanataaluma wote wa sheria nchini salamu nyingi za rambirambi kwa kuondokewa na mwenzao.”

Ameongeza: “Napenda vile vile kupitia kwako unifikishie pole nyingi kwa ndugu, jamaa na wanafamilia wa Marehemu Liundi ukiwajulisha kuwa niko nao katika masikitiko na majonzi ya msiba huu mkubwa. Wajulishe kuwa naelewa machungu yao katika kipindi hiki na namwomba Mwenyezi Mungu awape nguvu na subira kuweza kuvuka kipindi hiki kigumu. Aidha, naungana nao katika kumwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, ailaze peponi roho ya Marehemu George Liundi. Amen.”








All the contents on this site are copyrighted ©.