2014-01-16 11:03:09

Vatican inashiriki katika mkutano wa 65 wa Itifaki ya ulinzi kwa watoto duniani


Askofu mkuu Silvano Maria Tomasi, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Ofisi za Umoja wa Mataifa zenye makao makuu mjini Geneva, Alhamisi, tarehe16 Januari 2014, ameongoza ujumbe wa Vatican kwenye mkutano wa sitini na tano wa kimataifa unaojadili taarifa kutoka katika baadhi ya nchi wanachama yaani: Russia, Ujerumani, Ureno, Congo, Yemen na Vatican.

Hizi ni nchi ambazo zimewasilisha taarifa zake kama kielelezo cha utekelezaji wa Itifaki ya kulinda watoto iliyotiwa sahihi kunako Mwaka 1990, Vatican ikiwa pia ni kati ya nchi wanachama zilizotia sahihi Itifaki hii. Taarifa ya nchi husika inaonesha mahitaji ya sasa, kanuni msingi na mwongozo wa Itifaki hii. Kamati inaendelea kupitia taarifa za kila nchi mwanachama pamoja na kufanya majadiliano ya kina. Vatican inashiriki katika zoezi hili kama kielelezo makini kinachoonesha umuhimu wa Itifaki hii tangu ilipotiwa sahihi na nchi wanachama, kama jitihada za kulinda na kuwatetea watoto wadogo.

Vatican inaunga mkono juhudi za kuwalinda watoto dhidi ya nyanyaso na dhuluma na kwamba, wahusika wote wanapaswa kufikishwa mbele ya sheria ili kujibu shutuma zinazowakabili na kwamba, Vatican si kikwazo cha utekelezaji wa sheria kama ambavyo baadhi ya watu wamekuwa wakishutumu.

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kukazia kwamba, haki inapaswa kutekelezwa katika misingi ya ukweli na uwazi. Vatican kwa upande wake, itaendelea kutekeleza Itifaki ya kulinda Watoto pamoja na kufanyia kazi ushauri utakaotolewa na Kamati ya Itifaki katika mkutano wake wa sitini na tano huko Geneva.

Baba Mtakatifu amekwisha anzisha Tume ya Kulinda na Kutetea watoto. Kumbe, ushauri utakaotolewa na wajumbe, utafanyiwa kazi, ili kuliwezesha Kanisa kuendelea kutoa huduma makini kwa watoto katika Majimbo mbali mbali duniani. Vatican pamoja na mambo mengine inakazia umuhimu wa elimu na majiundo makini kwa watoto pamoja na kuzingatia makuzi na malezi yao: kiroho na kimwili kwa ajili ya watoto wote duniani.







All the contents on this site are copyrighted ©.