2014-01-16 07:38:20

Ujumbe wa Papa Francisko kwa ajili ya Siku ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani kwa Mwaka 2014


Hali ya wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum inahitaji kuangaliwa kwa usawa na ukamilifu zaidi, kwa njia ya ushirikiano wa kimataifa unaosimikwa katika mshikamano na huruma. RealAudioMP3

Hiki ndicho kiini cha ujumbe wa Siku ya 100 ya Wakimbizi na Wahamiaji inayoadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 19 Januari. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Mwaka 2014 unaongozwa na kauli mbiu “Wahamiaji na wakimbizi: kuelekea ulimwengu bora zaidi”.

Baba Mtakatifu Francisko anasema kuna mwingiliano mkubwa wa watu katika medani mbali mbali za maisha kwani watu wanapania kuboresha hali ya maisha ya binadamu katika masuala ya kiuchumi, kisiasa na kitamaduni. Kila mtu ni sehemu ya mchakato huu unaoleta matumaini kwa maisha bora zaidi kwa siku za usoni. Mchakato wa uhamiaji ni sehemu ya alama za nyakati hizi.

Ni kweli kwamba, uhamiaji umeonesha kasoro kubwa kwa nchi hisani na Jumuiya ya Kimataifa katika ujumla wake, lakini wahamiaji wanapaswa kufurahia umoja na heshima hata katika tofauti zake, kwa kupokelewa na kuonjeshwa ukarimu, ili kushirikishana rasilimali ya dunia, kwa kulinda utu na heshima ya binadamu; unaopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza.

Baba Mtakatifu anasema, Wakristo wanaangalia uhamiaji kama kielelezo cha kinzani kati ya uzuri wa kazi ya uumbaji, iliyonakishiwa na neema pamoja na ukombozi bila kusahau uwepo wa dhambi. Mshikamano, hali ya kupokelewa, udugu na kuelewana ni mambo yanayokwenda sanjari na kukataliwa, kubaguliwa, biashara haramu ya binadamu na unyonyaji, mateso na kifo.

Jambo linalosikitisha ni pale ambapo wahamiaji wanalazimika kuyakimbia makazi na nchi zao bila ya utashi wao binafsi; hali ambayo inachangia pia biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo. Utumwa wa kazi ni jambo ambalo kwa sasa linaendelea kuwa ni la kawaida kabisa. Licha ya matatizo na magumu yanayoendelea kuwakabili wahamiaji na wakimbizi, bado kuna wimbi kubwa la watu wanaotamani kupata maisha bora zaidi, kwa ajili yao, familia, ndugu na jamaa zao.

Dhana ya ujenzi wa ulimwengu bora zaidi inajikita katika maendeleo endelevu; kwa kufanya maboresha ya maisha ya watu; kwa kutoa majibu muafaka kwa matarajio ya watu binafsi na familia zao sanjari na kuhakikisha kwamba, kazi ya Uumbaji inaheshimiwa, inathaminiwa na kutunzwa. Lengo likiwa ni kuwa na uhakika wa chakula, tiba makini, fursa za ajira pamoja na uwajibikaji wa mtu binafsi, kwa kujifunza zaidi ili kupata zaidi.

Maendeleo ya kweli hayajioneshi kwa ukuaji wa uchumi peke yake, bali pale mahitaji ya mtu: kiroho na kimwili yanayopopewa kipaumbele cha kwanza, bila kuwabeza maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii; kwa kujenga utamaduni wa kukutana na kuwapokea, kwani wahamiaji na wakimbizi ni sehemu ya watoto wa Mungu wanaokimbia nchi zao kwa sababu mbali mbali. Hili ni kundi linaloweza kusaidia mchakato wa Uinjilishaji Mpya. Ndiyo maana Kanisa katika mikakati yake ya shughuli za kichungaji linapaswa kuwashirikisha wakimbizi na wahamiaji katika maisha na utume wa Kanisa.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa siku ya Wahamiaji na Wakimbizi anasema kwamba, licha ya maendeleo makubwa yanayojionesha sehemu mbali mbali za dunia, lakini bado kuna umaskini mkubwa wa hali na kipato, kuna vita, unyonyaji, ubaguzi, mateso, misimamo mikali ya kidini na kiimani. Haya ni kati ya vielelezo vya umaskini vinavyopaswa kufanyiwa kazi na Jumuiya ya Kimataifa.

Kuna uhusiano mkubwa kati ya tatizo la uhamiaji na umaskini; madhulumu na nyanyaso zinazowafanya baadhi ya watu kukimbia nchi zao, wakitafuta maisha bora zaidi; lakini kwa bahati mbaya, wanapofika ugenini wanakumbana na hali ya kutoaminiwa, kukataliwa na kutengwa mambo yanayoacha majeraha makubwa katika utu na heshima yao kama binadamu.

Tatizo la Wahamiaji na Wakimbizi linapaswa kushughulikiwa na Jumuiya ya Kimataifa kwa njia ya ushirikiano, mshikamano na huruma katika ngazi mbali mbali. Kuna haja ya kuwa na sera na sheria zinazopania kumlinda na kumwendeleza mwanadamu. Jambo hili linaweza kutekelezwa kwa kuwa na ushirikiano wa karibu kati ya nchi wanamotoka wahamiaji na wakimbizi na nchi zile zinazotoa hifadhi; sheria za kimataifa hazina budi kutumika kuratibu ili kulinda haki msingi za kila mhamiaji na mkimbizi pamoja na familia yake pamoja na kuzingatia sheria za nchi zinazotoa hifadhi.

Jamii ijitahidi kuondoa vikwazo visivyo vya lazima pamoja na kuendeleza mchakato wa kujenga na kudumisha usawa katika ulimwengu wa utandawazi. Jumuiya ya kimataifa iendeleze mchakato wa maboresho ya uchumi na hali ya kijamii katika nchi wanamotoka wahamiaji na wakimbizi hawa ili kwamba, uhamiaji isiwe ni dhana pekee kwa watu wanaotafuta: haki, amani, usalama na utu na heshima kama binadamu. Sera makini za kiuchumi zisaidie kutengeneza fursa za ajira na kwamba, jitihada za makusudi zifanywe ili familia za wahamiaji na wakimbizi ziweze kuishi kwa pamoja, ili kufurahia mshikamano na utulivu.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, kuna haja ya kuondokana na mawazo “mgando” dhidi ya wahamiaji na wakimbizi, ambao wanapojaribu kuomba uraia kama wakimbizi wa kisiasa wanakumbana na hali ya kudhaniwa vibaya pamoja ukinzani mkubwa, kwa kisingizio cha usalama wa raia; watachangia ukosefu wa fursa za ajira kwa wenyeji na “eti” wahamiaji na wakimbizi wanaweza kupoteza utambulisho na utamaduni wao,na hatimaye, vitendo vya jinai vitaweza kuongezeka.

Baba Mtakatifu Francisko anatoa changamoto kwa vyombo vya upashanaji habari kusaidia kufichua makosa yanayofanywa na baadhi ya watu, kwa kuendelea kuonesha pia ukweli, ukarimu na utu wema unaofanywa na kundi kubwa la wananchi. Umefika wakati wa kuwaonjesha wahamiaji na wakimbizi utamaduni wa kukutana ili kujenga dunia inayosimikwa katika haki na udugu. Vyombo vya habari vinapaswa pia kuongoka ili kutoa taswira nzuri ya wahamiaji na wakimbizi, kuliko wanavyotendewa kwa sasa.

Baba Mtakatifu anakumbuka jinsi ambavyo Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu ilivyolazimika kukimbilia uhamishoni ili kuokoa maisha ya Mtoto Yesu. Kanisa linatumwa ulimwenguni kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa kuwakumbatia wote, ndiyo maana Kanisa liko mstari wa mbele kulinda na kutetea utu na heshima ya kila binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Wahamiaji na wakimbizi ni ndugu wanaopaswa kusaidiwa na kushirikishwa katika mchakato wa Uinjilishaji Mpya.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, wahamiaji na wakimbizi katika safari yao ya maisha, watakutana na watu wenye moyo wa ukarimu, watakaowaonjesha mshikamano wa kidugu na joto la upendo wa kirafiki.

Ujumbe huuu umehaririwa na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.