Parokia ya Moyo Mtakatifu ya Yesu inajiandaa kumpokea na kuadhimisha Fumbo la Ekaristi
Takatifu na Papa Francisko! Yaani, we acha tu!
Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili jioni tarehe 19 Januari 2014, Siku ya Wahamiaji
na Wakimbizi Duniani, anatarajiwa kutembelea na kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu
kwenye Parokia ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, iliyoko Jimboni Roma. Baba Mtakatifu atapata
fursa ya kukutana na Familia ya Mungu, Parokiani hapo pamoja na maskini, wahamiaji
na wakimbizi wanaohudumiwa kila siku Parokiani hapo kama kielelezo cha upendo na mshikamano
na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.
Padre Valerio Baresi, Paroko wa
Parokia ya Moyo Mtakatifu wa Yesu iliyojengwa na Mtakatifu Yohane Bosco kunako Mwaka
1881 na kuwekwa chini ya usimamizi wa Shirika la Wasalesiani, anasema, walimwandikia
barua Baba Mtakatifu wakimwomba atembelee Parokia yao kwani ni kati ya Parokia ambazo
ziko pembezoni mwa Jiji la Roma, kama kielelezo cha upendo na mshikamano na maskini,
wanaotafuta kuonja huruma na upendo kutoka kwa Kristo na Kanisa lake.
Baba
Mtakatifu akiwa Parokiani hapo atapata nafasi ya kuwaungamisha baadhi ya waamini watakaokuwa
wamejiandaa kwa ajili ya kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani zao, changamoto ya
kuthamini na kupokea Sakramenti ya Upatanisho, ili kuonja huruma na upendo wa Mungu.
Waamini wanaendelea kujiandaa kiroho na kimwili ili kukutana na hatimaye kuadhimisha
Fumbo la Ekaristi Takatifu na Baba Mtakatifu Francisko! Wanasema, Parokiani hapo hapatoshi!
Yaani we acha tu!