2014-01-16 14:56:48

Papa atema cheche! Kashfa ndani ya Kanisa ni kielelezo cha imani haba!


Kashifa nyingi zinazotokea ndani ya Kanisa ni kutokana na viongozi wa Kanisa kutoweka kipaumbele cha kwanza katika: Sala na Tafakari ya Neno la Mungu linalopaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha sanjari na kujenga uhusiano wa dhati kabisa na Mwenyezi Mungu.

Kanisa litashindwa kutekeleza utume na dhamana yake, ikiwa kama viongozi wake watashindwa kuwa waaminifu kwa Mwenyezi Mungu. Waisraeli katika Agano la Kale walishindwa na Wafilisti, kwa sababu walikuwa wamekengeuka na kumwacha Mwenyezi Mungu. Neno la Mungu ambalo ni dira na taa katika maisha ya watu wa Mungu halikupewa tena kipaumbele na kudhani kwamba, kwa kuchukua Sanduku la Agano, ingeweza kuwa kinga yao dhidi ya Wafilisiti.

Lakini wakashangaa kuona kwamba, hata pamoja na kuwa na Sanduku la Agano, kielelezo cha uwepo wa Mwenyezi Mungu kati yao, walishindwa vibaya na kukumbana na maafa makubwa, kiasi hata cha Sanduku la Agano kuchukuliwa na Wafilisti. Hii inatokana na ukweli kwamba, Waisraeli kwa wakati ule hawakuwa na imani thabiti kwa Mwenyezi Mungu na wala hawakuthamini uwepo wake endelevu kati yao.

Hayo yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Ibada ya Misa Takatifu siku ya Alhamisi, tarehe 16 Januari 2014 kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican. Baba Mtakatifu anasema kwamba, mahali ambapo kumetokea kashfa na makwazo ndani ya Kanisa ni kielelezo kwamba: Imani, Sala, Tafakari ya Neno la Mungu ni mambo ambayo yalikuwa ni haba katika maisha ya wahusika, walikuwa na nguvu ya kiuchumi na ufahari, lakini Neno la Mungu lilitundikwa pembeni mwa maisha ya watu hao!

Baba Mtakatifu anawasihi viongozi wa Kanisa kuhakikisha kwamba, wanatoa Neno la uzima linalofumbata ukweli kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao ya kila siku. Kwa njia hii, Familia ya Mungu itaweza tena kubahatika kuiona sura ya Kristo na Mwenyezi Mungu atawakumbuka katika shida na taabu zao. Waamini wanapaswa kuwa ni waaminifu kwa Neno la Mungu na sheria zake vinginevyo wanaweza kukiona kilicho mnyoa Kanga manyoya!







All the contents on this site are copyrighted ©.