2014-01-16 08:24:43

Khalifa wa Mtakatifu Petro si kikwazo cha majadiliano ya kiekumene bali ni daraja linalounganisha juhudi za kiekumene!


Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuimarisha majadiliano ya kiekumene miongoni mwa Wakristo na kwamba, hivi ni kati ya vipaumbele vyake katika maisha na utume wa Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo.

Hivi ndivyo anavyobainisha Kardinali Kurt Koch, Rais wa Baraza la Kipapa la kuhamasisha umoja wa Wakristo, wakati huu Wakristo wanapojiandaa kuanza Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo kwa Mwaka 2014, unaongozwa na kauli mbiu " Je, Kristo amegawanyika? Sehemu ya Waraka wa kwanza wa Mtakatifu Paulo kwa Wakorintho 1: 1-17. Itakumbukwa kwamba, Juma la kuombea Umoja wa Wakristo lianza tarehe 18 hadi tarehe 25 Januari, Siku kuu ya Kuongoka kwa Mtume Paulo mwalimu wa Mataifa.

Kardinali Koch anasema, tema hii inakwenda sanjari na hija ya sala ya Baba Mtakatifu Francisko katika Nchi Takatifu kuanzia tarehe 24 hadi tarehe 26 Mei 2014, kama kumbu kumbu ya Maadhimisho ya Miaka 50 tangu Papa Paulo VI alipotembelea Nchi Takatifu. Akiwa huko, Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kukutana na kuzungumza na Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox.

Juhudi zinaendelea kufanyika ili kuangalia uwezekano wa Baba Mtakatifu Francisko kukutana na kuzungumza na Patriaki Kiril wa Moscow, Russia. Kama wazo hili litaweza kuzaa matunda yanayokusudiwa, hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa Papa kukutana na kuzungumza na Patriaki wa Kanisa la Kiorthodox la Russia.

Kardinali Kurt Koch anasema, tangu baada ya Maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, Viongozi wakuu wa Kanisa wameendelea kutoa kipaumbele cha kwanza kwa umoja na mshikamano wa Kanisa kwa kukazia majadiliano ya kiekuemene, ili Wakristo wawe wamoja chini ya Kristo mchungaji mkuu. Kumbe, kuhusu dhamana na nafasi ya Khalifa wa Mtakatifu Petro katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene si kikwazo bali ni daraja linalounganisha juhudi za Kiekumene.







All the contents on this site are copyrighted ©.