2014-01-16 07:46:53

Jumapili ya kuombea amani nchini Uingereza


Amani ya kweli inapata chimbuko lake katika maisha ya mtu, kuanzia ndani ya Familia na hapo amani hii inaweza kusambaa na kueneza harufu nzuri ya manukato kwa jirani na jamii nzima. RealAudioMP3

Huu ndio mwaliko unaotolewa na Chama cha kitume cha Amani kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza, Pax Christi, katika Maadhimisho ya Jumapili ya amani nchini Uingereza itakayofanyika hapo tarehe 19 Januari 2014.

Maadhimisho haya yataongozwa na Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya Siku ya 47 ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2014, unaongozwa na kauli mbiu “udugu ni msingi na njia ya amani. Baraza la Maaskofu linawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kusali kwa ajili ya kuombea familia zao, Jumuiya za Kiparokia, ili ziweze kuheshimiana, kuthaminiana na kusaidiana kama ndugu wamoja.

Maaskofu wanawaalika waamini kusali pia kwa ajili ya Kanisa la kiulimwengu, ili watu waweze kuonesha mshikamano wa dhati katika mapambano dhidi ya umaskini, njaa na maradhi yanayoendelea kunyanyasa na kutesa mamillioni ya watu duniani. Pax Christi inayaelekeza maombi yake kule Mashari ya Kati, kwa ajili ya kuombea: haki, amani na upatanisho wa kitaifa; ili kweli watu waweze kuvunjilia mbali kishawishi cha chuki na uhasama na kuanza kujikita katika misingi ya ukweli, haki na amani mintarafu Injili ya Kristo.

Waamini wanahimizwa kuendelea kumwombea Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake, ili kweli aweze kuwa ni chombo cha umoja na mshikamano wa Kanisa, linalopania kukoleza imani, matumaini na mapendo miongoni mwa Familia ya Mungu duniani. Watu wajifunze na kutamani kutoka katika undani wa mioyo yao kutembea katika mwanga wa amani, kwa njia ya ushuhuda wa mshikamano kwa wale wanaoteseka kutokana na baa la njaa, umaskini, hali ngumu na kukosefu wa fursa za ajira, mambo ambayo kwa sasa ni “majanga” ya familia nyingi duniani.

Waamini na watu wenye mapenzi mema, wawe na ari na mwamko wa kusimama kidete kulinda na kutetea haki msingi za binadamu kwa kukata taa katu katu nyanyaso na dhuluma katika viunga vyao! Ni changamoto ya kuwasaidia wanafunzi ambao wanashindwa kuendelea na masomo yao kutokana na hali ngumu ya maisha! Jumuiya ziguswe na mahangaiko yao, ili hatimaye, kujipanga kikamilifu kuwasaidia wanafunzi hao kwa kuwekeza katika elimu kwa ajili ya maboresho ya maisha yao kwa siku za usoni!

Kimsingi, Jumapili ya kuombea amani, iwe ni chachu ya kujenga misingi ya haki, amani na mshikamano wa kweli miongoni mwa watu kwa njia ya ushuhuda wa imani katika matendo!








All the contents on this site are copyrighted ©.