2014-01-15 11:11:39

Siku 21 za Kufunga na Kusali kwa ajili ya kuombea amani Sudan ya Kusini


Askofu Baran Eduardo Hiiboro Kussala wa Jimbo la Tombura-Yambio, Sudan ya Kusini, anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuungana pamoja kwa ajili ya kusali ili kuombea amani na utulivu nchini Sudan ya Kusini ambayo kwa sasa inakabiliana na vita ya wenyewe kwa wenyewe.

Hiki ni kipindi cha Siku 21 kilichoanza tarehe 12 Januari 2014, Sherehe za Ubatizo wa Bwana na kitakamilika tarehe 2 Februari 2014, Siku kuu ya Kutolewa Bwana Hekaluni, sanjari na Siku ya Watawa Duniani. Hizi ni siku za Sala na kufunga ili kumlilia Mwenyezi Mungu aweze kuwakirimia tena amani na utulivu.

Askofu Kussala anakumbusha kwamba, kadiri ya takwimu za kihistoria inaonesha kwamba, kuna watu millioni 4.5 walifariki dunia wakati wa kupigania uhuru nchini Sudan, changamoto na mwaliko wa kuifahamu na kukumbatia historia, ili watu wasirudie tena makosa yaliyopita kwa kujikita katika amani inayopata chimbuko lake kutoka katika undani wa maisha ya mwanadamu.

Fedha na chakula ambacho waamini na watu wenye mapenzi mema watajinyima wakati wa kufunga ili kuombea amani, kitapelekwa kusaidia watu wenye shida zaidi, kama kielelezo cha mshikamano a upendo na waathirika wa vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan ya Kusini.







All the contents on this site are copyrighted ©.