Padre Henri de la Kethule hivi karibuni ameiomba Serikali ya DRC pamoja na wadau wengine
kuhakikisha kwamba, wanakomesha biashara haramu ya watoto inayoendelea kushamiri katika
miji ya Kikwit na Kinshasa nchini DRC. Kwa zaidi ya miezi tisa sasa biashara haramu
ya watoto imeendelea kufanywa na baadhi ya watu wenye uchu wa mali na utajiri wa haraka
haraka katika mkoa wa Bandundu.
Padre Henri
de la Kethule ameyasema hayo wakati alipokuwa anazungumza na Radio Okap kwa kukazia
kwamba, kuna baadhi ya watu wanatumia mgongo wake kutokana na huduma anayoitoa kwa
ajili ya watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi kupata watoto ambao baadaye wanawatumbukiza
katika biashara haramu ya watoto, jambo ambalo linakwenda kinyume kabisa cha haki
msingi za binadamu, uhuru na ustawi wa watoto hao kwa siku za usoni.
Baadhi
ya watu hao wanawalaghai wazazi wa watoto wanaoishi katika hali ya umaskini kuwapatia
watoto wao ili waweze kuwatunza na kuwawezesha kupata kesho iliyo bora zaidi mjini
Kinshasa, kumbe, lengo ni kutaka kuwauza kwenye soko la biashara haramu ya binadamu
ambalo kwa sasa linashika kasi ya ajabu mjini Kinshasa anasema Padre Henri de la Kethule.
Wazazi wengi wanadhani kwamba, watoto wao watapelekwa na kutunzwa kwenye nyumba
za watoto yatima, kumbe, ukweli wa mambo ni kwamba wanauzwa kama bidhaa mjini Kinshasa.
Padre Henri anawataka viongozi wa Serikali na wadau mbali mbali kusimama kidete kusitisha
biashara ya binadamu nchini DRC, kabla hawajachelewa!