Mshikamano, umoja na udugu ni mambo yanayopania kulinda na kutetea utu na heshima
ya binadamu katika misingi ya haki na amani!
Askofu mkuu Silvano Maria Tomasi, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Ofisi za
Umoja wa Mataifa zilizoko mjini Geneva anasema kwamba, Vatican itaendelea kuhamasisha
utamaduni wa kujadli, kuthamini na kulinda utu na heshima ya binadamu dhidi ya utamaduni
wa kifo na hali ya kutojali wala kuthamini watu wengine katika shida na mahangaiko
yao.
Kwa njia hii, Jamii itaweza kuanza mchakato wa ujenzi wa Jamii inayosimikwa
katika umoja, upendo na mshikamano wa kidugu, kama anavyohimiza Baba Mtakatifu Francisko.
Umefika wakati wa kuchuchumilia Injili ya Uhai na kuachana kabisa na matumizi ya silaha
kama njia ya kutatua mataizo ya kisiasa na kijamii yanayozikabili nchi nyingi duniani
kama inavyojitokeza huko Syria.
Vyombo vya upashanaji habari visaidie mchakato
wa kuelimisha Jamii umuhimu wa kuheshimiana, kuthaminiana na kusaidiana kwa hali na
mali. Tofauti za imani na dini; rangi na kabila zisiwe ni chanzo cha vita na kinzani
za kijamii; watu watambue kwamba, wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mwenyezi Mungu;
tofauti zao ni utajiri unaopaswa kuthaminiwa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi.
Udugu ni msingi na njia ya kujenga na kudumisha amani kwa kushinda kishawishi
cha migawanyiko ya Kijamii, Ubinafsi, uchu na uroho wa mali na madaraka. Ikumbukwe
kwamba, vita itaendelea kuwa ni chanzo kikuu cha uvunjifu wa misingi ya haki na kwamba,
vita inasababisha mateso na mahangaiko ya kwa watu wasiokuwa na hatia.
Askofu
mkuu Silvano Maria Tomasi anabainisha kwamba, mchango wa wawakilishi wa Vatican kwenye
Umoja wa Mataifa na Mashirika mbali mbali mbali ya Kimataifa unapania kuhamasisha
Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu;
kujenga na kuimarisha ushirikiano na mshikamano wa kidugu unaosimikwa katika kanuni
ya auni, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi.
Askofu mkuu Silvano Maria
Tomasi anasema jitihada za kutafuta amani huko Mashariki ni za siku nyingi zinazofanywa
na Jumuiya ya Kimataifa. Vita inayoendelea nchini Syria ni matokeo ya kinzani za kivita
nchini Iraq, hali ambayo inasababisha mateso na usumbufu mkubwa kwa mamillioni ya
watu wasiokuwa na hatia huko Syria.
Jambo la msingi kwa sasa, Jumuiya ya Kimataifa
inataka wahusika wa mgogoro wa kivita nchini Syria kusimamisha mapigano ambayo yanaendelea
kusababisha majanga kwa wananchi wengi na kuanza majadiliano, ili kuweza kupata suluhu
na amani ya kudumu. Jumuiya ya Kimataifa ina matumaini makubwa kwa Awamu ya Pili ya
Mkutano kwa ajili ya Syria huko Geneva.