Mkakati wa Makanisa ya Kiluteri katika kulinda na kutunza mazingira!
Shirikisho la Makanisa ya Kiluteri Duniani kwa Mwaka 2014 linawaalika waamini na watu
wote wenye mapenzi mema kushiriki katika kampeni ya kulinda na kutunza mazingira kama
sehemu ya kazi ya uumbaji kwa kufunga walau siku moja kwa kila mwezi, tangu Januari
2014 hadi Mwezi Desemba, 2014, wakati ambapo kutaanza mkutano kuhusu Mazingira huko
Lima, PerĂ¹. Kwa njia hii,
Shirikisho la Makanisa ya Kiluteri Duniani linataka kuwashirikisha waamini wake na
watu wote wenye mapenzi mema, kufanya tafakari ya kina kuhusu umuhimu wa utunzaji
bora wa mazingira, kama sehemu ya Maandalizi ya Mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu
mabadiliko ya tabianchi unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa Mwaka 2014 huko Lima,
PerĂ¹. Viongozi wakuu wa Shirikisho hili wanasema, wameamua kufunga na kusali kila
mwezi, kama njia ya kuonesha mshikamano wao na waathirika wa mabadiliko ya tabianchi
sehemu mbali mbali za dunia. Kuna mamillioni ya watu wameathirika kutokana na athari
za mabadiliko ya tabianchi sehemu mbali mbali za dunia. Hii itakuwa ni nafasi pia
kwa ajili ya kuwakumbuka wanaofariki dunia kutokana na majanga asilia. Lengo kuu
ni kujaribu kuwaunganisha waamini na watu wenye mapenzi mema ili waweze kujenga hoja
ya nguvu ili kusaidia katika mchakato wa kulinda na kutunza mazingira. Kufunga na
kusali ni tendo la maisha ya kiroho, lakini lina faida yake hata katika maisha ya
kawaida. Uamuzi huu ulifikiwa hapo tarehe 18 Desemba 2013. Siku ya kwanza ya mfungo
na sala, ilikuwa ni hapo tarehe Mosi, Januari 2014. Kufunga na kusali ni kuwashirikisha
wengine tunu msingi za maisha ya kiroho. Ni changamoto ya kufanya magezu katika mitindo
ya maisha kwa kusoma alama za nyakati. Kwa mwamini ni fursa ya kufanya toba na kuomba
msamaha wa dhambi; tayari kuwajibika barabara katika kulinda na kutunza mazingira
kwa ajili ya mafao ya wengi. Athari za mabadiliko ya tabianchi ni changamoto ambayo
inaendelea kufanyiwa kazi na Shirikisho la Makanisa ya Kiluteri Duniani na ni sehemu
ya mkakati wake wa shughuli za kichungaji kuanzia Mwaka 2012 hadi Mwaka 2017. Lengo
ni kujitahidi kupata haki ya tabianchi sanjari na utunzaji bora wa mazingira, kwa
ajili ya kizazi hiki na kile kijacho, ili watu waweze kuwa na afya njema.