Mabalozi na wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa wanaunga mkono jitihada za Papa
Francisko katika kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu!
Jumuiya ya Kimataifa inakabiliana na changamoto kubwa kutokana na ongezeko la watu
wanaokabiliana na baa la njaa duniani, wahamiaji na wakimbizi wanaotafuta usalama
na ubora wa maisha; biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo; nyanyaso na madhulumu
dhidi ya Wakristo sehemu mbali mbali za dunia. Wanadiplomasia wanakubaliana kimsingi
na changamoto hii inayoendelea kutolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika utume na
maisha ya Kanisa.
Hayo yamesemwa na Balozi Jean-Claude Michel, Dekano wa Mabalozi
wanaoziwakilisha nchi zao mjini Vatican wakati alipokuwa anatoa salam za matashi mema
kwa Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican, Jumatatu tarehe 13 Januari 2014 wakati
Mabalozi walipokutana na Baba Mtakatifu Francisko.
Mabalozi wanampongeza Baba
Mtakatifu kwa kuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi mambo yote yanayotaka kufisha
utu na heshima ya binadamu katika medani mbali mbali za maisha. Mabalozi wameahidi
kwamba, watafikisha kilio cha Baba Mtakatifu Francisko kwa Serikali zao, ili kukifanyia
kazi kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi, utu na heshima ya binadamu vikipewa
kipaumbele cha kwanza.
Balozi Jean- Claude Michel amegusia vita na kinzani
za kijamii zinazotokana na misimamo mikali ya kidini na hali ya kutovuliana; mambo
ambayo yameendelea kusababisha majanga makubwa kwa maisha ya watu sehemu mbali mbali
za dunia. Anasema, Waraka wa kitume wa Baba Mtakatifu Francisko Injili ya Furaha,
Evangelii Gaudium ni muhimu sana katika mchakato wa majadiliano ya kidini miongoni
mwa waamini wa dini mbali mbali, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani,
upendo na upatanisho wa kweli.
Balozi Michel anasema, majanga asilia yaliyojitokeza
sehemu mbali mbali za dunia kwa kiasi kikubwa yanachangiwa na binadamu mwenyewe kwa
kutopea katika ubinafsi; kwa kutozingatia misingi ya amani, haki na usawa ndani ya
Jamii. Baadhi ya watu wameelemewa mno na uchu wa mali, hali ambayo imeendelea kusababisha
vita, kinzani na uharibifu mkubwa wa mazingira. Kuna mamillioni ya watu wanaolazimika
kuzikimbia nchi zao kutokana na sababu mbali mbali, hawa nao wanapaswa kuhudumiwa
kikamilifu.
Mabalozi na wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa mjini Vatican
ameahidi kuunga mkono jitihada za Baba Mtakatifu Francisko katika mchakato unaopania
kuifanya dunia kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi; kwa kusimama kidete kulinda
na kutetea utu na heshima ya binadamu; uhuru wa kidini. Uhusiano wa Vatican na Jumuiya
ya Kimataifa umekuwa na manufaa makubwa kwa ajili ya mafao ya wengi. Mwaka 2015, Vatican
itakuwa inasherehekea Jubilee ya Miaka 50 tangu ilipoanzisha uhusiano wa Kidiplomasia
na Umoja wa Mataifa.