2014-01-14 07:39:36

Barua ya Papa kwa Makardinali wateule!


Baba Mtakatifu Francisko amewaandikia barua Makardinali wateule kwa kuwahakikishia uwepo wake wa karibu kwa njia ya sala, baada ya kuteuliwa kuwa washiriki na wasaidizi wa karibu wa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Anawaalika kwa namna ya pekee Makardinali kujivika karama na matamanio ya Yesu Kristo, ili waweze kushiriki kikamilifu katika kumsaidia Baba Mtakatifu kutekeleza wajibu na dhamana yake kwa Kanisa la Kiulimwengu.

Baba Mtakatifu anawakumbusha Makardinali wapya kwamba, kwa kuteuliwa kwao kuwa Makardinali si kwamba, wamepandishwa cheo na kupewa heshima, bali ni huduma inayowataka kuwa na mwelekeo na moyo mpana zaidi. Ni changamoto ya kuwa na mwono mpana na kupenda wote, kwa njia ya unyenyekevu kwa kujifanya kuwa mtumishi wa wote.

Baba Mtakatifu anawaalika kupokea uteuzi wake kama jambo la kawaida kwa moyo wa unyenyekevu. Wajitahidi kuonesha furaha yao mintarafu moyo wa kiinjili kwa kujinyima, kiasi na kuzingatia fadhila ya ufukara.

Baba Mtakatifu anawakaribisha kwa mikono miwili hapo tarehe 20 Februari 2014, watakapoanza siku mbili za tafakari ya kina kuhusu Familia. Baba Mtakatifu anahitimisha barua yake kwa kujiweka mbele yao wakati wowote watakapomhitaji na kwamba, waendelee kumsindikiza katika maisha na utume wake kwa njia ya Sala.








All the contents on this site are copyrighted ©.