Wazazi wana dhamana na wajibu wa kurithisha imani kwa watoto wao!
Katika Sherehe ya Ubatizo wa Bwana inayofunga rasmi Kipindi cha Noeli, Baba Mtakatifu
Francisko alitoa Sakramenti ya Ubatizo kwa watoto 32: kati yao kuna wasichana 18 na
wavulana 14. Ibada hii ya Misa takatifu imeadhimishwa kwenye Kikanisa cha Sistina,
kilichopo mjini Vatican.
Baba Mtakatifu katika mahubiri yake anasema kwamba,
Yesu hakuwa na sababu msingi za kubatizwa na Yohane Mbatizaji, lakini kutokana na
Umungu wake, aliweza kuyatakatifuza maji yote kiasi kwamba, yanaweza kutumika kwa
Sakramenti ya Ubatizo. Tangu wakati huo, Sakramenti ya Ubatizo imeendelea kutolewa
na Mama Kanisa kwa watoto wake wanaozaliwa kwa Maji na Roho Mtakatifu. Watoto hawa
waliobatizwa watakuwa na dhamana ya kurithisha imani ya Kikristo kwa watoto wao katika
siku za usoni.
Baba Mtakatifu Francisko amekazia kwamba, wazazi na walezi wanalo
jukumu nyeti la kuhakikisha kwamba, wanarithisha imani ya Kikristo kwa watoto wao.
Huu ndio urithi mkubwa wanaoweza kuwaachia watoto wao hapa duniani. Watoto hawa kwa
sauti na kilio chao wanamwinulia Mungu wimbo wa sifa na shukrani. Baba Mtakatifu amewataka
akina mama kuwanyonyesha watoto wao bila woga wowote kwani katika tukio hili wao ndio
wahusika wakuu.