Vatican itaendelea kushirikiana na wadau mbali mbali katika ujenzi wa udugu na upendo
kati ya watu kiini cha maridhiano na amani!
Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 13 Januari 2014 amekutana na kuzungumza
na Mabalozi pamoja na wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa mjini Vatican kwa kuwatakia
kheri na baraka kwa Mwaka mpya wa 2014. Amekumbuka kwa namna ya pekee Hayati Balozi
Alejandro Valladares Lanza, aliyekuwa dekano wa Mabalozi kwa miaka mingi, aliyefariki
dunia hivi karibuni.
Baba Mtakatifu anasema, mwaka 2013 umesheheni matukio
makubwa katika maisha na utume wa Kanisa. Katika masuala ya Kidplomasia Vatican imefanya
mikataba ya uhusiano wa kimataifa na nchi kama: Sudan ya Kusini, Cape Verde, Hungari,
Chad pamoja na kuridhia mkataba na nchi ya Guinea Equatorial, kunako mwaka 2012. Vatican
inaendelea kuwa na wawakilishi katika Mashirikisho ya Kimataifa huko Amerika ya Kusini,
Asia na Barani Afrika, hususan katika Jumuiya ya Uchumi kwa Nchi za Afrika Magharibi,
ECOWAS.
Baba Mtakatifu anasema, udugu kama msingi na njia ya amani ni changamoto
inayopata chimbuko lake tangu mtu anapozaliwa tumboni mwa mama yake, kimsingi, dhana
hii ya upendo inapaswa kujidhihirisha katika moyo wa huduma ili kujenga na kuimarisha
amani bila ubaguzi, kila mtu akijitahidi kutekeleza wajibu wake, kwani familia ndio
kiini na msingi wa amani. Lakini familia nazo zinaendelea kukabiliana na hali ngumu
kiasi hata cha kukosa mahitaji msingi, jambo linalohitaji sera makini zitakazosaidia
kuimarisha misingi bora ya kifamilia.
Baba Mtakatifu anasema, vijana na wazee
ni tumaini la Jamii kwani wao ni hazina ya hekima na mang'amuzi ya maisha na vijana
wanao mwelekeo wa maisha kwa siku za usoni. Kuna haja ya kuwekeza kwa vijana ili waendelee
kuwa na matumaini kwa kesho iliyo bora zaidi. Baba Mtakatifu anasema, ameyaona matumaini
ya vijana wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani huko Rio de Janeiro. Vijana
walisali na kuonesha ari na mwamko wa kukumbatia maisha kwa kuendelea kushirikiana
na vijana wenzao, changamoto ya kujenga utamaduni wa kukutana, ili kuimarisha umoja,
furaha pamoja na kudumisha amani.
Baba Mtakatifu anasema, Mwaka uliopita ulisheheni
matukio yanayokumbatia utamaduni wa kifo, unaojidhihirisha katika: ubinafsi, chuki
na uhasama; uchu wa mali na madaraka. Inaonekana kana kwamba, hali hii limekuwa ni
jambo la kudumu. Kwa Wakristo, Noeli ni siku kuu ya kuzaliwa kwa Mfalme wa amani anayegeuza
ubafsi kuwa ni sehemu ya majitoleo binafsi na kisasi kugeuzwa kuwa ni kielelezo cha
msamaha.
Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, Mwaka 2014 utakuwa
ni Mwaka wa amani na Syria ambayo anaendelea kuipatia kipaumbele cha pekee kwa sala
na kufunga itaonja tena amani na utulivu. Anawashukuru wote wanaounga mkono juhudi
za kutafuta amani nchini Syria na kwamba, tarehe 22 Januari 2014 utakuwa ni mwanzo
wa mchakato wa upatanisho; kwa kuheshimu na kuthamini haki msingi za binadamu na kwamba,
raia wasiokuwa na hatia wataendelea kulindwa. Baba Mtakatifu anatoa mwaliko kwa Jumuiya
ya Kimataifa kuendelea kutoa msaada wa kibinadamu kwa wananchi wa Syria na nchi jirani
kama vile Lebanon na Jordan zinazotoa msaada kwa wakimbizi na wahamiaji kutoka Syria.
Katika hotuba yake, Baba Mtakatifu ameonesha wasi wasi kuhusu hali ya kisiasa
na kijamii nchini Lebanon jambo linaloweza kuhatarisha amani na utulivu huko Mashariki
ya Kati. Kuna haja ya kuwa na makubaliano ya kisiasa na kijamii nchini Misri na huko
Iraq watu wakijikite zaidi katika kudumisha utulivu na amani. Papa ameridhika na hatua
iliyofikiwa katika majadiliano kuhusu silaha za nyuklia kati ya Iran na Kundi la Nchi
5 kujumlisha Moja. Kuna umuhimu wa kujenga na kudumisha utamaduni wa majadiliano yanayoongozwa
na nguvu ya kimaadili na haki badala ya kukimbilia matumizi ya mtutu wa bunduki.
Baba
Mtakatifu anasema, Jumuiya ya Kimataifa Mwaka huu inaadhimisha Kumbu kumbu ya Miaka
100 tangu ilipotokea Vita kuu ya Kwanza ya Dunia, changamoto ya kulinda na kuheshimu
utu kwa kuthamini hata tofauti zinazojitokeza kati ya watu. Majadiliano ya amani kati
ya Israeli na Palestina hayana budi kuendelezwa kwa mchango wa Jumuiya ya Kimataifa
ili kupata suluhu na amani ya kudumu.
Bado inasikitisha kuona kwamba, kuna
Wakristo wanaokimbia kutoka Mashariki ya Kati na Afrika ya Kaskazini. Hawa ni watu
wanaopaswa kushiriki katika ujenzi wa nchi zao katika medani mbali mbali za maisha,
kwa kutafuta daima mafao ya wengi, haki, amani na upatanisho wa kitaifa.
Baba
Mtakatifu anasema, Wakristo katika baadhi ya nchi wanalazimika kutolea ushuhuda wa
upendo na huruma ya Mungu, hata pale wanapodhulumiwa na kuteswa katika nchi zao wenyewe,
kama inavyojitokeza nchini Nigeria, Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati ambao wanaendelea
kukabiliana na utamduni wa kifo. Ni matumaini yake kwamba, Jumuiya ya Kimataifa itawasaidia
wakimbizi na hatimaye, kusitisha vita na kinzani katika nchi hizi; tayari kuanza mchakato
wa upatanisho, haki na amani kati ya wananchi wote. Upatanisho na amani ni mambo ambayo
yanapaswa kupewa kipaumbele hata katika Nchi nyingine za Kiafrika; hususan, Mali na
Sudan ya Kusini.
Vatican inayo matumaini makubwa kwamba, Jubilee ya uhusiano
kati ya Vatican na Korea kitakuwa ni kichocheo upatanisho kwa ajili ya mafao ya wananchi
wa Korea katika ujumla wao, kwa ajili ya mafao ya wengi. Kuna haja ya kuendeleza utamaduni
wa kuheshimiana, ushirikiano na amani Barani Asia. Misimamo mikali ya kidini haina
budi kudhbitiwa na uhuru wa kidini kuheshimiwa na wote. Vatican itaendelea kushirikiana
na nchi mbali mbali duniani kwa ajili ya kujenga na kuimarisha mafao ya wengi.
Baba
Mtakatifu anasema, bado kuna vita, njaa na magonjwa mambo yanayokuzwa zaidi kutokana
na utandawazi wa kutojali shida na mahangaiko ya wengine sanjari na kukumbatia utamaduni
wa kifo kwa sera za utoaji mimba na watoto kupelekwa vitani kwa kunyanyaswa na kudhalilishwa
utu na heshima yao. Bado kuna kundi kubwa la watoto linalotumbukizwa katika biashara
haramu ya binadamu na utumwa mamboleo.
Kuna mamillioni ya watu wanaokimbia
nchi zao kutokana na majanga asilia na vita hasa kwenye nchi zilizoko kwenye Pembe
ya Afrika na Eneo la Maziwa Makuu. Kuna wakimbizi wanaotambulikana kwa namba na wala
si katika utu wao! Hali hii inajionesha pia Amerika ya Kusini wanaokimbilia nchini
Marekani bila kuwasahau Wahamiaji wanaotoka Afrika wakitafuta maisha bora zaidi Barani
Ulaya, lakini wengi wao wanakufa maji hata kabla ya kufika Ulaya, kama inavyojionesha
kwenye Visiwa vya Lampedusa, Kusini mwa Italia. Wote hawa ni watu wanaohitaji kuonjeshwa
moyo wa ukarimu na mshikamano.
Baba Mtakatifu anasema, kuna haja kwa Jumuiya
ya Kimataifa kulinda na kutunza mazingira kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa amani.
Baba Mtakatifu anawaalika wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa na wadau mbali mbali kuhakikisha
kwamba, wanatunga sera makini zitakazolinda na kutunza mazingira. Uharibifu mkubwa
wa mazingira umeendelea kuwa ni chanzo kikubwa cha maafa asilia sehemu mbali mbali
za dunia.
Baba Mtakatifu anahitimisha hotuba yake kwa Mabalozi na Wawakilishi
wa Jumuiya ya Kimataifa kwa kuwakumbusha kwamba, amani inajengwa kila siku ya maisha,
kwa kuzingatia haki. Hii ndiyo dhamana inayotekelezwa na Mama Kanisa katika maisha
na utume wake, sehemu mbali mbali za dunia kwa kumhudumia mtu mzima: kiroho na kimwili,
ili watu wengi zaidi waweze kuonja huruma na upendo wa Mungu. Vatican itaendelea kushirikiana
na nchi mbali mbali katika ujenzi wa udugu na upendo kati ya watu, kiini na msingi
wa maridhiano na amani kati ya watu!