2014-01-13 08:49:48

Tambueni uzuri wa imani, ili muweze kushiriki kikamilifu katika Sakramenti za Kanisa na Maisha ya Kijumuiya!


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Sherehe ya Ubatizo wa Bwana, Jumapili tarehe 12 Januari 2014, amemshukuru Mwenyezi Mungu kwa ajili ya watoto 32 waliozaliwa kwa Maji na Roho Mtakatifu, kielelezo cha imani na furaha ya Familia ya Mungu. Kwa Ubatizo wa Bwana, kwenye Mto Yordani, mbingu na dunia zilifunguka na kuleta matumaini mapya kwa binadamu.

Ujio wa Mwana wa Mungu hapa duniani ulikuwa ni mwanzo wa uwepo wa huruma na upendo wa Mungu kwa watu wake, baada ya mbingu kufungwa kutokana na dhambi na hivyo kuweka kizingiti kati ya binadamu na Muumba wake. Kwa kuzaliwa kwa Yesu Kristo Mwana wa Mungu, anasema Baba Mtakatifu, mbingu zilifunguka tena na Mwenyezi Mungu akawapatia binadamu upendo wa kweli na kufungua mbingu, tukio lililoshuhudiwa na wachungaji kule kondeni mjini Bethlehemu; Mamajusi kutoka Mashariki ya mbali, Yohane Mbatizaji, Mitume wa Yesu na Mtakatifu Stefano, Shahidi wa kwanza kuyamimina maisha yake kwa ajili ya Injili.

Baba Mtakatifu anasema, tukio hili linaweza kuonekana na waamini wengine hata leo huii, ikiwa kama wataukumbatia upendo wa Mungu, waliokirimiwa kwanza kabisa walipopokea Ubatizo kwa njia ya Roho Mtakatifu. Yesu kwa kukubali kubatizwa Ubatizo wa toba, alionesha mshikamano wa dhati na wadhambi waliokuwa wanafanya hija ya toba na wongofu wa ndani.

Kwa njia ya Ubatizo, Mwenyezi Mungu anamtambulisha Mwanaye Mpendwa Yesu Kristo aliyependezwa naye! Kwa njia hii Yesu anashiriki kwa ukamilifu ubinadamu na umaskini wake, ili aweze kuwapenda pasi na ukomo, kiasi cha kuwaita ndugu zake, licha ya mapungufu yao ya kibinadamu. Pamoja na Yesu, wanafanyika kuwa ni watoto wateule wa Mungu.

Baba Mtakatifu anasema, huu ni wakati wa huruma ya Mungu, kila mwamini anapaswa kuwa na kiu ya kutaka kushirikisha udugu na upendo wake kwa wengine, kwa vile anaguswa na mahangaiko pamoja na shida za jirani zake. Kwa njia hii maisha yanapata ladha na mwelekeo mpya. Anawaalika waamini kumwomba Bikira Maria ili aweze kuwaombea kwa Mwanaye wa pekee, waweze kumfuasa Kristo katika njia ya imani na upendo inayofunguliwa mbele yao kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo.

Mwishoni Baba Mtakatifu Francisko amewakumbuka kwa namna ya pekee, wazazi na walezi waliobatiza na wale wote watakaowabatiza watoto wao, kuendeleza furaha ya Ubatizo na kwamba, Sakramenti hii iwasaidie wazazi na walezi kutambua tena uzuri wa Imani, ili hatimaye, kushiriki kikamilifu katika maisha ya Kisakramenti na kwenye Jumuiya ya Kikristo.







All the contents on this site are copyrighted ©.