2014-01-13 10:05:07

Mwanaharakati na mtetezi wa walemavu akutana na Papa Francisko


Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 11 Januari 2014 alikutana na kuzungumza na Mheshimiwa Ileana Argentin, mlemavu na mwanaharakati anayefahamika sana kwa kutetea haki za walemavu Jijini Roma na katika Bunge la Italia.

Mheshimiwa Ileana alikuwa amemwandikia barua Baba Mtakatifu Francisko, kumwomba ili aweze kukutana naye ili kumshirikisha kuhusu hali ya walemavu na baada ya kitambo kifupi, Baba Mtakatifu aliweza kumjibu na kumpatia nafasi ya kukutana naye Jumamosi iliyopita, mazungumzo ambayo yamedumu kwa takribani nusu saa.

Akielelezea kuhusu mkutano huu, Padre Federico Lombardi, msemaji mkuu wa Vatican anabainisha kwamba, Mheshimiwa Ileana amemwomba Baba Mtakatifu asaidie harakati za kuwawezesha wazazi wenye watoto wenye ulemavu ili waweze kutekeleza wajibu na dhamana yao kwa heshima na hali ya kiutu, kuliko hali ilivyo kwa sasa. Wasi wasi ni kuhusu hali ya watoto walemavu pale wanapofiwa na wazazi wao, wanajikuta katika mazingira magumu zaidi kwani hata wakati mwingine wanashindwa kupata huduma kutoka kwa ndugu zao wa karibu.

Mheshimiwa Ileana amegusia pia vikwazo wanavyokumbana navyo walemavu kutokana na miundo mbinu mingi ambayo bado haijatoa kipaumbele kwa watu wenye ulemavu.

Baba Mtakatifu Francisko kwa upande wake, ameguswa na mchango wa Ileana Argentin, amemhakikishia uwepo wake wa karibu ili kuwatia moyo wanaharakati wanaosimama kidete kulinda na kutetea haki za walemavu, ili Jamii iweze kujihusisha zaidi kuyatafutia ufumbuzi matatizo wanayokumbana nayo!








All the contents on this site are copyrighted ©.