2014-01-13 07:29:24

Jiwekeeni miiko ili kujenga na kulinda maisha yenu ya ndoa na familia!


Mpendwa msikilizaji wa Radio Vatican, kwa mara nyingine tena karibu katika kipindi chetu pendevu cha Kanisa la nyumbani. Lengo letu: tunataka kuunganisha nguvu za pamoja katika kuzijenga na kuzichunga familia zetu vema, familia ambazo ni Kanisa la nyumbani. RealAudioMP3
Kanisa linataka familia zetu ziwe shule, shule ya upendo, shule ya utii, shule ya uaminifu, shule ya sala, na hata shule ya kazi, na shule ya fadhila nyingi. Kumbe sote tusaidiane, kuandaa mazingira ya familia ili kweli yawe ya mwanadamu kufunzwa na kujifunza tunu mbalimbali za utu wema. Kutoka humo, mwanadamu aandaliwe kuwa tunu kwa Kanisa na kwa taifa na kwa familia nzima ya mwanadamu.

Katika kipindi kilichopita tuliangazia Nyanja tatu za maandalizi ya kuupokea wito wa ndoa na kujenga Kanisa la nyumbani, yaani familia. Kabla hatujaangazia ushiriki wa jamii katika maandalizi hayo; kwanza tukazie maarifa kwa waoanaji wenyewe. Baada ya kufanya kila aina ya maandalizi; kwa hakika wanajua kabisa kwamba wanaingia katika maisha mapya, yenye majukumu mapya tena mazito.

La muhimu kabisa hapa ni kutunza hadhi na heshima ya maisha ya ndoa na familia. Ili hilo liweze kutimizwa vema, wajifunze sasa kujiwekea miiko. Miiko hapa, tuelewe kama makatazo binafsi na mipaka unayojiwekea mwenyewe ili usilete harufu mbaya au ukakasi katika mahusiano ya ndani ya ndoa. Miiko hiyo ipo mingi sana. Kwetu sisi, tuitazame WALAO MITANO.

Mosi, MWIKO WA MAHUSIANO: Ndugu, wewe sasa umekuwa mke wa mtu au mume wa mtu; angalia sana aina ya watu unaohusiana nao. Maisha ya ndoa ni maisha ya watu wakomavu tu. Ukomavu huo uonekane pia katika kudhibiti mahusiano yako na watu. Kuna watu ambao walikuwa marafiki zako zetu kabla hatujaingia katika agano, mlikuwa mnashinda pamoja, mnakula na kunywa siku nzima hadi asubuhi.

Wewe ni mtu wa ndoa sasa; KUNA BAADHI YA MARAFIKI ITABIDI UWASADAKE TU, weka umbali nao au uwaache kabisa.. Wapo wengine wanaofaa sana, lakini wengine hawafai, watakuharibia ndoa yako; kwa maneno yao na matendo yao. LA MSINGI NI KWAMBA UNAHUSIANA NA NANI, KWA NINI NA HADI WAPI. Wewe ni mume wa mtu! Sasa unajisahau, kila wakati upo na wasichana wengine mnakula na kunywa, unamwacha mwenzio kulinda nyumba. Au eti kila siku upo kazini hadi saa za usiku, na ukitoka huko, unapitiliza kwenda bar kupoteza mawazo; unarudi nyumbani ukiwa hauna mawazo tena. Yote yamepotelea bar. Hapo hautajenga Kanisa la Nyumbani.

Pili , MWIKO WA MAZINGIRA: Mtu wa ndoa, tunza heshima yako. Usipende kuwa kila mahali. Kuna mazingira mengine ile kuonekana tu; tayari utaleta mashaka ya lazima; hata kama hujafanya kosa, kuonekana tu hapo ni tatizo. Wewe kila siku upo vijiweni baba, unafanya nini? Mama, kila siku uko nyumba za waganga wa vienyeji; au unaonekana ukitoka kwenye nyumba za wageni. Hutawasadikisha watu wote kwamba ulikwenda kumsalimu mjomba. Mazingira tu, yanatia wasiwasi. JILINDE!!

Tatu, MWIKO WA MAVAZI: Jambo hili litazamwe kwa hekima yote. Siku hizi kunajengeka utamaduni wa kutopenda nguo. Kuna vijivazi vifupi au vinavyobana sana. Hizi fasheni zisituibie utu na heshima yetu. Wewe ni mke wa mtu sasa, kuna mavazi mengine hayakufai kabisa kuvaa hadharani. Utaalika dharau au utaalika wahuni wafikiri kwamba na wewe bado ni mmoja wao.

Baba wa familia, mume wa mtu kabisa , amening’iniza suruali nusu mlingoti, utadhani anajiandaa kuchomwa sindano; hapana!! Mavazi huweza kupendekeza tabia ya mtu. Usikubali jamii ikakuweka katika kundi ambalo halikuhusu kwa kuwa mzembe katika mavazi.

Nne, MWIKO WA VYAKULA NA VINYWAJI: Leo hii katika utaratibu wetu wa soko huria katika ulimwengu wa watu ambao wanajali zaidi pesa kuliko uhai na utu wa watu; tuwe macho, vyakula vingi havifai na vipo ambavyo vinaharibu kabisa hata miundombinu ya ndoa na familia. Hili tutalifafanua kitaalamu kwa wakati wake. Lakini tuseme pia juu ya kiasi katika matumizi ya pombe. Kwa ujumla wake, ULEVI NI SUMU KUBWA KATIKA NDOA. Ndoa za walevi hazina amani hata siku mmoja. Baba akilewa anarudi na MATUSI, KELELE NA KUWA MKOROFI TU, watoto wanasikia na wanaona. Mama naye akirudi amelewa, NI KELELE NA MATUSI YA KILA AINA.

Mwisho ulevi unawapelekea kwenye madeni makubwa, baadaye madeni yanawafanya wauze hata vitu vya familia, na huku familia itaendelea kuteseka. JE HADI HAPO ULEVI UNA THAMANI GANI? Ndugu, CHA MUHIMU NI KWAMBA USITAMADUNISHE ULEVI. Wanaume wasome YBS. 19:1-3.

Tano, MWIKO WA MAWASILIANO: Ndugu wewe ni mke wa mtu au mume wa mtu; yakupasa kuwa mwangalifu na watu unaowasiliana nao, iwe ana kwa ana au kwa kutumia vyombo vya mawasiliano hasa SIMU. Usipende kuwasiliana na kila mtu, hata pasipo sababu za msingi. NDOA ZA WATU WENGI ZIMEJERUHIWA KWA SABABU YA SIMU. Usipowadhibiti rafiki zako juu ya mawasiliano, wataandika UJUMBE WENYE MATATA utakaoleta fujo katika ndoa yako. Sio lazima kila mtu awe na namba yako ya simu.

Na sio lazima uwepo katika mitandao yoote na kijamii. Sio busara sana kupenda kupiga picha na kila mtu au kupigwapigwa picha kila mahali na kila mtu. Wewe hujawa maua! Ipo siku picha hizo zitaning’inizwa katika mitandao na safari ya ndoa yenu itachechemea tu. Wengi siku hizi tumepoteza dhamiri ya uadilifu, hatuoni haya kuwaharibia wengine maisha.

Mpendwa msikilizaji, mambo haya tutayaangazia tena tutakapohekimishana juu ya ushiriki wa jamii katika maandalizi na katika kuifanya ndoa changa ianze kwa mwondoko unaostahili. Sote kama jumuiya tunawajibika kulijenga Kanisa la nyumbani.


Kwa leo tunaishia hapa; hadi kipindi kijacho, kutoka katika Studio za Radio Vatican, ni Mimi Padre Pambo Martin Mkorwe OSB.







All the contents on this site are copyrighted ©.