Hata Makanisa maskini na machanga yanayo uwezo wa kuchangia katika maisha na utume
wa Kanisa la kiulimwengu
Padre Federico Lombardi Msemaji mkuu wa Vatican akifafanua kuhusu uteuzi wa Makardinali
wapya uliofanywa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili iliyopita, tarehe 12 Januari
2014 anasema kwamba, Papa Francisko ameendelea kufuata sheria ya kuwa na Makardinali
120 walio chini ya miaka 80 wenye haki ya kupiga na kupigiwa kura wakati wa uchaguzi
wa Khalifa wa Mtakatifu Petro.
Baba Mtakatifu ameamua kuteuwa Makardinali
16 wenye haki ya kupiga na kupigiwa kura. Kati ya Makardinali wateule, 4 ni wale wanotekeleza
dhamana na utume wao mjini Vatican. Makardinali wengine 12 ni Maaskofu wakuu wanaoishi
katika Majimbo yao sehemu mbali mbali za dunia. Kimsingi, Baba Mtakatifu ameteuwa
Makardinali 2 kutoka Ulaya; Amerika ya Kaskazini na Kati ni Makardinali 3, Amerika
ya Kusini walioteuliwa ni Makardinali 3. Bara la Afrika limepata Makardinali wapya
3, hali kadhalika na Bara la Asia limepata Makardinali 2.
Baba Mtakatifu Francisko
kwa kuamua kuwateuwa Maaskofu wakuu: Phillippe Nakellentuba Ouèdraogo kutoka Jimbo
kuu la Ouagadougou, Bukrina Faso na Askofu Chibly Langlois, Jimbo la Les Cayes, Haiti
anaonesha upendeleo wa pekee kwa Makanisa maskini, ambayo hata katika umaskini wao,
bado yanaweza kuchangia katika maisha na utume wa Kanisa la Kiulimwengu. Hawa ni Makardinali
wanaopaswa kuwa mabalozi wema katika mapambano dhidi ya umaskini, ujinga na maradhi.
Baba
Mtakatifu ameamua pia kuteuwa Makardinali katika Majimbo ambayo kimsingi si Majimbo
ya Kikardinali, kama ilivyotokea kwa Jimbo kuu la Perugia, Italia na Kisiwa cha Mindanao
nchini Ufilippini. Kati ya Makardinali wateule, wenye sifa ya pekee licha ya kuwa
na umri mkubwa ni Askofu mkuu mstaafu Loris Francesco Capovilla, mwenye umri wa miaka
98, ambaye alikuwa ni Katibu muhtasi wa Papa Yohane wa XXIII, anayetarajiwa kutangazwa
kuwa Mtakatifu, kama sehemu ya Maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 50 ya Mtaguso mkuu
wa Pili wa Vatican.
Padre Federico Lombardi anasema, Makardinali wapya ambaye
ni kijana kuliko wote ana umri wa miaka 55 ambaye ni Askofu Chilby Langlois kutoka
Jimbo la Les Cayes, Haiti. Na Kardinali mzee kuliko wote ni Askofu mkuu mstaafu Loris
Francesco Capovilla, mwenye umri wa miaka 98.