Askofu Nunzio Galantino, Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI anaendelea
kuhimiza umuhimu wa sala katika kulea na kukuza miito mitakatifu ndani ya Kanisa.
Huu ndio mwelekeo mpya unaotolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika kuhamasisha miito
mitakatifu ndani ya Kanisa, jambo ambalo linapaswa kuvaliwa njuga na idara za kichungaji.
Hivi karibuni,
Baraza la Maaskofu Katoliki Italia liliendesha kongamano la miito mitakatifu lililokuwa
linaongozwa na kauli mbiu “Jiweke wazi katika ukweli, utakuwa na maisha. Miito ni
ushuhuda wa maisha”. Mikakati ya kichungaji kuhusiana na miito haina budi kutoa kipaumbele
cha kwanza katika maisha ya sala, kwani bila sala kazi yote ya kuhamasisha miito ni
bure! Ni sawa na “kumpigia mbuzi gitaa ukimtegemea aserebuke” anasema, Askofu Nunzio
Galantino.
Sala na ushuhuda wa maisha ni chanda na pete, kwani haya ni mambo
yanayotegemeana. Mapadre na watawa wawe ni mifano bora ya kuigwa katika maisha na
matendo yao, ili vijana wanapowaona waweze kuvutika kujitoa bila ya kujibakiza kwa
ajili ya Mungu na jirani zao kwa njia ya Kanisa. Ushuhuda huu ujikite katika ile furaha
inayobubujika kutoka katika undani wa maisha ya Padre au mtawa, kama anavyokazia Baba
Mtakatifu Francisko.
Kwa njia hii, Kanisa litaweza kuwapata Mapadre na Watawa
ambao si wafanyakazi wa mshahara, watu wanaojitafuta wenyewe kwa ajili ya masilahi
yao binafsi, bali ni watu wanaomwamini Yesu Kristo, kiasi cha kujitoa bila ya kujibakiza
kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Mapadre na watawa katika ushuhuda wa maisha yao
wawe ni watu wanaopenda na kusimamia ukweli. Maisha yao yawe ni kielelezo cha ushuhuda
wa ukweli wanaoufundisha, kuutangaza na kuumwilisha katika vipaumbele vya maisha yao
ya kila siku. Unafiki ni sumu ya miito mitakatifu.
Kwa upande wake, Monsinyo
Nico Dal Molin, mkurugenzi wa Idara ya miito, Baraza la Maaskofu Katoliki Italia anasema
kwamba, kuna haja ya kutangaza na kushuhudia ukweli katika ulimwengu mamboleo ambamo
watu wanapendelea kujikita katika “umbea” ambao kimsingi si mtaji na mambo yasiokuwa
na mashiko wala mafao ya wengi. Watu wajifunze kutafuta ukweli, kuzingatia umuhimu
wa maisha na kwamba, ukweli hauna mjadala, daima una gharama ambayo inapaswa kulipwa!
Dunia inahitaji mashahahidi wanaoshuhudia ukweli na uwazi; mambo msingi yanayobubujika
kutoka katika undani wa mtu mwenyewe! Kwa kupenda na kuthamini ukweli, kuna maanisha
ya kuwa ni watoto wa mwanga wanaotembea katika Mwanga wa ukweli ambao ni Yesu Kristo
mwenyewe. Ni watu wanaofahamu na kuthamini upendo, tayari kuwashirikisha wengine.
Kwa njia hii waamini wanaweza kuwa ni mwanga wa mataifa unaofukuza giza la ubaya na
dhambi.