2014-01-11 11:09:01

Rais Kikwete azungumza na Mabalozi pamoja na wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa, Ikulu, Dar es Salaam


Jumuiya ya Kimataifa ilikuwa na kila sababu ya kusherehekea maziko ya Hayati Mzee Nelson Mandela, aliyefariki dunia Mwezi Desemba 2013 nchini Afrika ya Kusini. Ni kiongozi aliyejipambanua kwa kupigania haki msingi za binadamu sanjari na utokomezaji wa utawala wa ubaguzi wa rangi nchini Afrika ya Kusini. Hali ya Tanzania kwa sasa ni shwari na Serikali itaendeleza mapambano dhidi ya biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya pamoja na kuzidisha mapambano dhidi ya rushwa.

Tanzania itaendelea kuimarisha mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha Mwaka 2013 na kwamba, uchumi wa nchi unatarajiwa kukua kwa asilia 7.3 katika Kipindi cha Mwaka 2014 pamoja na kudhibiti mfuko wa bei, ingawa kuna baadhi ya maeneo nchini Tanzania yanayokabiliwa na uhaba wa chakula. Serikali inapania kuendeleza maboresho ya huduma ya maji mijini na vijijini; udhibiti wa ugonjwa wa malaria, Ukimwi pamoja na vifo vya watoto wadogo chini ya umri wa miaka mitano. Tanzania pia inapania kuendeleza mchakato wa ugavi wa umeme mijini na vijijini, ili kufikia asilimia 30% ifikapo mwaka 2015.

Haya ni kati ya mambo makuu yaliyozungumzwa na Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania katika halfa ya kuukaribisha Mwaka Mpya 2014 aliyowaandalia Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa nchini Tanzania, hapo tarehe 10 Januari 2014 Ikulu, Jijini Dar es Salaam.

Anasema, Rasimu ya Pili ya Katiba ya Tanzania itajadiliwa na Bunge Maalum kwa muda kati ya siku 70 na siku 90 na hapo Rasimu ya Katiba ya Tanzania itapelekwa kwa wananchi ili ipigiwe kura ya maoni. Tanzania inasherehekea Jubilee ya Miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar na Miaka 50 ya Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar, uliounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Rais Kikwete anasema kwamba, Serikali yake inaendelea kushirikiana na nchi nyingine Kikanda na Kimataifa, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi hasa katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi. Ni matumaini ya Serikali ya Tanzania kwamba, itaendelea kushirikiana na wadau mbali mbali katika mchakato wa maendeleo endelevu nchini Tanzania na Afrika kwa ujumla.







All the contents on this site are copyrighted ©.