Majibu ya maswali dodoso kuhusu changamoto za maisha ya ndoa na familia ni kielelezo
cha utamaduni wa majadiliano ndani Kanisa
Baraza la Maaskofu Katoliki Uswiss limepata majibu kutoka kwa waamini wapatao 23,
000 waliojibu maswali dodoso yaliyotolewa na Baraza la Kipapa la Familia kama sehemu
ya mchakato wa Maandalizi ya Maadhimisho ya Sinodi Maalum ya Maaskofu kuhusu Familia,
itakayoadhimishwa mjini Vatican, kuanzia tarehe 5 hadi tarehe 19 Oktoba, 2014.
Maaskofu wanasema,
majibu kutoka kwa waamini na watu wenye mapenzi mema yamevuka matarajio waliyokuwa
nayo mara baada ya kutoa maswali dodoso, kielelezo cha mwanzo wa utamaduni wa majadiliano
ya kina kuhusu maswala nyeti ya maisha na utume wa Kanisa ili kujenga na kuimarisha
uhusiano mwema na hali ya kuaminiana kati ya waamini na viongozi wa Kanisa
Maswali
dodoso yalijikita zaidi na zaidi kuhusu mikakati ya kichungaji kwa wanandoa, tunu
msingi za maisha ya kifamilia na changamoto zake; na jinsi ambavyo Kanisa linaweza
kuwasaidia wanandoa kutekeleza dhamana na wajibu wao ndani ya Kanisa na Jamii katika
ujumla wake.
Waamini wengi nchini Uswiss wanamshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu
Francisko kwa kuguswa na mateso pamoja na mahangaiko ya wanandoa sehemu mbali mbali
za dunia, kiasi cha kutoa kipaumbele cha kwanza katika utume na maisha yake, jambo
linalojionesha kwa kuitisha Sinodi Maalum ya Maaskofu kwa ajili ya Familia na sala
kwa ajili ya kuombea Familia.
Waamini wanachangamotishwa na Mama Kanisa kushiriki
kikamilifu kujibu maswali dodoso yatakayosaidia kutengeneza hati ya kutendea kazi
wakati wa Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Familia, ijulikanayo kwa
lugha ya Kilatini kama “Instrumentum Laboris”.