Huduma makini kwa watu wa Mungu ni sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji Mpya!
Caritas na Uinjilishaji mpya ndiyo kauli mbiu iliyoongoza semina ya thelathini na
saba ya Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki nchini Cameroon iliyoanza tarehe 6 Januari
hadi tarehe 11 januari 2014 mjini Douala, Cameroon. Semina hii ilianza
kwa Ibada ya Misa Takatifu iliyoadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Mitume Petro na Paulo
na kuwashirikisha: Maaskofu, Mapadre, Watawa na Waamini walei kutoka sehemu mbali
mbali za Cameroon. Maadhimisho haya ni muhimu sana katika maisha na utume wa Familia
ya Mungu nchini Cameroon, wakati huu Kanisa Barani Afrika linapoendelea kujiwekea
mikakati ya Uinjilishaji Mpya kwa njia ya huduma makini zinazotolewa katika sekta
mbali mbali za maisha. Haya ni maneno ya Monsinyo Sebastien Mongo Behon, Katibu
mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Cameroon, ambaye pamoja na mambo mengine amekazia
umuhimu wa Kanisa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni
mwa Jamii. Hawa ni wagonjwa, maskini, watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi,
wakimbizi, wahamiaji na wote wanaoteseka kutokana na sababu mbali mbali katika maisha.
Kwa upande wake, Askofu mkuu Samuel Kleda, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki
Cameroon anasema, Kanisa halina budi kuzivalia njuga kero zinazowakabili waamini na
wananchi wa Cameroon katika ujumla wake, kwa kuangalia kwa kina na mapana dhamana
na utume wa Caritas Cameroon katika mchakato wa kukabiliana na changamoto hizi. Lengo
ni kutaka kuhakikisha kwamba, Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki, Caritas linakuwa
ni kichocheo kikuu cha Uinjilishaji Mpya kwa njia ya huduma makini kwa maskini na
wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Caritas ni kielelezo cha upendo na mshikamano
unaobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake ! Huduma za kijamii na kiuchumi ziwe
ni kielelezo cha mchango wa Kanisa katika harakati za kumkomboa mwanadamu: kiroho
na kimwili, tayari kumwonjesha Injili ya Furaha. Kanisa halina budi kutoa kipaumbele
cha kwanza kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii kama alivyofanya
Kristo mwenyewe na kama ambavyo Baba Mtakatifu Francisko anavyoendelea kuhimiza katika
maisha na utume wa Kanisa. Naye Bwana Michael Roy, Katibu mkuu wa Shirikisho la
Misaada la Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis anasema, Uinjilishaji
Mpya ni mchakato unaopania kuliwezesha Kanisa kurithisha Imani ya Kikristo, kama ilivyoelekezwa
na Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kuhusu Uinjilishaji, iliyoadhimishwa Mjini Vatican
kunako Mwaka 2012. Huduma ya upendo kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni
mwa jamii ni asili ya Kanisa, kwani hakuna Uinjilishaji Mpya pasi na huduma makini,
kielelezo cha ushuhuda wa imani tendaji. Imani inayomwilishwa katika huduma ya upendo
inaleta mguso mkubwa kwa watu wanaoipokea, kwani huu ni ushuhuda wa upendo wa Mungu
kwa ajili ya watu wake pasi na upendeleo. Ni huduma inayowawezesha waamini kuwa ni
Wamissionari wa Habari Njema ya Wokovu kwa kujiinjilisha kwanza wao wenyewe! Mama
Kanisa anatambua mchango unaotolewa na wadau mbali mbali katika mchakato wa Uinjilishaji
Mpya, lakini huduma ya upendo na mshikamano wa kidugu ina kishindo kikuu katika maisha
ya watu. Haitoshi kufahamu mbinu na mikakati ya Uinjilishaji Mpya, bali jambo la msingi
ni kutambua ikiwa kama wadau wenyewe wa Injili ni mashahidi wanaoaminiwa na kuthaminiwa
na Jamii inayowazunguka!