2014-01-11 08:08:06

Changamoto za kichungaji baada ya Maadhimisho ya Mwaka wa Imani


Bwana tuongezee imani, ndiyo kauli mbiu inayoongoza barua ya kichungaji ya Patriaki Fouad Twal wa Yerusaleme katika kufunga Mwaka wa Imani, uliotangazwa na kuzinduliwa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI, ukaendelezwa na hatimaye kufungwa rasmi na Papa Francisko kwa kishindo kikubwa, sanjari na Maadhimisho ya Sherehe za Kristo Mfalme wa Ulimwengu. RealAudioMP3

Mwaka wa Imani kimekuwa ni kipindi ambacho kimetoa changamoto kwa waamini kukiri, kuadhimisha, kuishi na kushirikisha wengine Furaha ya Injili.

Ni mwaka ambao uliosheheni matukio makubwa katika maisha na utume wa Kanisa. Ni mwaka ambao umeshuhudia Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita aking’atuka kutoka madarakani kwa utashi kamili na kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa la Kristo. Familia ya Mungu ikashuhudia Papa Francisko, mtu wa watu akichaguliwa kuliongoza Kanisa kama Khalifa wa Mtakatifu Petro; kiongozi anayeendelea kuwashangaza wengi kutokana na unyenyekevu na mikakati yake ya kichungaji inayotoa kipaumbele cha kwanza kwa: Mungu, Kristo, Kanisa na binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko ni kiongozi anayeonesha cheche za mwendelezo wa mageuzi ndani ya Kanisa, ili kufikia utimilifu wa maisha ya Kikristo, yaani utakatifu. Mlango wa Imani, Mwanga wa Imani na Injili ya Furaha ni nyaraka ambazo zina umuhimu wa pekee katika maisha na utume wa Kanisa, lakini kwa namna ya pekee, katika mchakato wa Uinjilishaji Mpya unaojikita katika imani tendaji inayotolewa ushuhuda na waamini katika uhalisia wa maisha.

Patriaki Twal anasema kwamba, imani ni fadhila ya Kimungu ambayo kwayo waamini wanamsadiki Mungu na kila kitu alichokisema, alichofunulia, na ambacho Kanisa Takatifu linawataka waamini kusadiki, kwa sababu Mungu ndiye kiini cha ukweli wenyewe. Imani ni mwanga angavu unaowangazia mwamini ili asitembee katika dhambi na uvuli wa mauti. Imani inamwezesha mwamini kufanya maamuzi ya busara kwa wakati muafaka pamoja na kuendelea kutambua mapenzi ya Mungu. Hii ni zawadi na nguvu kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ili kutekeleza utashi wake.

Imani ni hazina kubwa kwa waamini wanaoishi katika Nchi Takatifu, kwani wao wamebahatika kuishi katika maeneo Yesu amezaliwa, ameishi, akateswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu ili kukamilisha kazi ya Ukombozi. Waamini wanapaswa kuwa ni mashahidi amini wa Kristo Mfufuka pasi na woga, hata kama wanaonekana kuwa ni kundi dogo, katika Nchi Takatifu.

Waamini wanakumbushwa kwamba, Mwenyezi Mungu ni mwaminifu kwa ahadi zake, changamoto kwa waamini pia kuwa waaminifu kwa Mwenyezi Mungu kama inavyojionesha katika Maandiko Matakatifu, lakini kwa namna ya pekee kwa Mzee Ibrahim, Baba wa Imani kamilifu, aliyejiachilia mikononi mwa tunza na ulinzi wa Mwenyezi Mungu katika mapito ya maisha yake.

Patriaki Twal anasema, imani inajionesha kwa namna ya pekee katika maisha ya Bikira Maria, aliyejitahidi kumwilisha imani katika matendo ya huruma kama inavyojionesha alipotoka kwa haraka kwenda kumhudumia binamu yake Elizabeth aliyekuwa mjamzito; walipolazimika kukimbilia nchini Misri ili kuokoa maisha ya Mtoto Yesu, aliposimama chini ya Msalaba akamwona Mwanaye wa pekee akiinamisha kichwa na kukata roho kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu.

Bikira Maria ni kielelezo cha imani thabiti, inayomkirimia mwamini amani, utulivu wa ndani na utakatifu wa maisha. Kimsingi anasema Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, imani inapaswa kujionesha katika matendo ya upendo ili kudumisha matumaini pasi na kukata tamaa.

Wakristo katika Nchi Takatifu wanakabiliana na hali ngumu ya maisha, wasi wasi na hata wakati mwingine wanaonja dalili za kukata tama. Waamini wanakumbushwa kwamba, Mwenyezi Mungu kwa njia ya Mwanaye Yesu Kristo atawafariji kwa njia ya imani, matumaini na mapendo.

Patriaki Twal anawaambia Wakristo kwamba, haitoshi kuzaliwa na kukulia katika Familia ya Kikristo, bali neema hii inapaswa kuendelezwa kwa kukubali kukutana na kumpokea Neno wa Mungu aliyefanyika mwili kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu, akawapatia neema ya kufanyika watoto wateul wa Mungu, changamoto ya kuendelea kumtolea ushuhuda wa maisha, kwa kuwaonjesha wengine Injili ya Furaha; Huruma na Upendo; kwa kusimama kidete kulinda na kutetea haki msingi za binadamu. Ni mwaliko wa kulinda na kutunza mazingira kwani hii pia ni sehemu ya kazi ya Uumbaji ambayo inaimba sifa ya matendo makuu ya Mungu.

Wakristo wanakumbushwa kwamba, Yesu Kristo ni Neno wa Mungu aliyefanyika mwili, katika mambo yote akawa sawa na binadamu ila hakutenda dhambi. Yesu Kristo amewafunuliwa watu sura ya Mungu inayojikita katika huruma na mapendo. Ni Bwana na Mwalimu aliyeonesha umabhiri wake katika Heri za Mlimani na kwenye Sala ya Baba Yetu. Ni mwaliko kwa waamini kuwa ni Kristo mwingine, ili watu waweze kuguswa na ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo! Tafakari ya Fumbo la Umwilisho linalopata hitimisho lake katika Fumbo la Pasakaa, hii ni fursa fursa ya kuona matendo makuu ya Mungu katika kazi ya Uumbaji na Ukombozi.

Kwa Wakristo, Yesu ni Mkombozi; ni Neno wa Mungu na sura ya Baba wa Milele, changamoto kwa waamini kujitaabisha kumfahamu, kumpenda na kumtumikia Kristo, ili awasaidie kuwaongoa na hatimaye, kuwawezesha kuwa ni watu wapya zaidi. Yesu ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; ni kielelezo cha Mtumishi mwaminifu, aliyethubutu kuyamimina maisha yake kwa ajili ya rafiki zake. Wakristo wakipenda wanaweza kufanya tafakari ya kina kuhusu maisha na utume wa Yesu unaosimuliwa kwa namna ya pekee katika Maandiko Matakatifu.

Biblia ni maktaba kubwa kuliko zote ulimwenguni, ina vitabu 46 vya Agano la Kale na Vitabu 27 kutoka katika Agano Jipya, waamini wajitaabishe kulisoma, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha. Neno la Mungu ni dawa ya maisha ya kiroho, ni shule ya utakatifu wa maisha na ukombozi wa mwanadamu.

Patriaki Twal katika barua yake ya kichungaji kama sehemu ya kufunga Mwaka wa Imani, anawakumbusha waamini kwamba, wanasukumwa kuamini katika Kanisa moja, takatifu, katoliki na la mitume. Hii ndiyo imani ambayo Mitume wameirithisha kwa waamini vizazi baada ya vizazi, changamoto kwa waamini kwa njia ya imani, kuchuchumilia utakatifu wa maisha, kwa toba na wongofu wa ndani. Watakatifu ni mifano bora ya kuigwa katika imani na nguzo rejea katika hija ya maisha ya hapa duniani. Hata leo bado kuna watakatifu wanaoendelea kutolea ushuhuda wa imani ka Kristo na Kanisa lake, sehemu mbali mbali za dunia.

Patriaki Twal anawaalika Wakristo kutolea ushuhuda wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, kwa kutambua kwamba, kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, kila Mkristo amepewa dhamana ya kuwa ni Mmissionari, tayari kujitosa kimasomaso kutangaza Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Hii ni imani inayojisimika katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, Kanisa na Mambo ya Nyakati.

Familia, Parokia na shule ziwe ni mahali pakutangaza na kurithisha, kukuza na kukomaza imani kwa njia ya: Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa na Matendo ya huruma. Mapadre na Watawa wanahamasishwa na Mama Kanisa kuwaimarisha ndugu zao katika imani, matumaini na mapendo, kwa kutambua kwamba, wao ni Wamissionari wenye dhamana ya kumhubiri Kristo hadi miisho ya dunia. Mara baada ya Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, Kanisa bado lina dhamana na utume wa kuendelea kutangaza Injili ya Furaha hadi miisho ya dunia.

Patriaki Twal anasema, tangu mwanzo damu ya mashahidi na wafiadini imekuwa ni mbegu ya Ukristo sehemu mbali mbali za dunia, hata leo hii bado kuna watu wanateseka kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Hii ni kutokana na misimamo mikali ya kiimani na baadhi ya watu kukosa utamaduni wa kuvumiliana. Wakristo kama raia wengine katika Nchi Takatifu wana haki ya kuishi hapa. Wakristo wajiandae kutoa sadaka hata ikibidi sadaka ya maisha yao, kama inavyoendelea kujitokeza sehemu mbali mbali huko Mashariki ya Kati.

Wakristo wanaalikwa kujitokeza kifua mbele ili kushiriki kikamilifu katika maisha ya hadhara na wala hakuna sababu ya kujitenga, kwani kuishi katika Nchi Takatifu ni neema na baraka na wala si laana. Wawe ni mashahidi amini wa Yesu Kristo Bwana na Mwalimu; kwa kutambua kwamba, wanayo dhamana ya kushiriki katika maisha na utume wa Kanisa, tayari kutolea ushuhuda wa hazina kubwa ya imani wanayoibeba katika mioyo yao!

Patriaki Fouad Twal wa Yerusalem anahitimisha Barua yake ya kichungaji kama sehemu ya mchakato wa kufunga Mwaka wa Imani kwa kuwataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuimarisha matumaini yao kwa Kristo na Kanisa lake; kwa kutolea ushuhuda wa imani tendaji sanjari na kutambua umuhimu wa imani katika maisha na utume wa Kanisa.

Maisha ya Mkristo yaendelee kutoa harufu ya utakatifu wa maisha, kwa njia ya toba na wongofu wa ndani; kwa kusimama kidete kulinda na kutetea misingi ya haki, amani, utulivu; maisha, utu na heshima ya binadamu. Waamini wawe ni mashahidi amini wa imani, matumaini na mapendo, kiasi hata cha kuyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake.

Kwa njia ya neema na baraka za Mwenyezi Mungu, Wakristo washinde kishawishi cha kutaka kuikimbia Nchi Takatifu kwa kuogopa madhulumu, bali waendelee kuwa ni chumvi na mwanga wa mataifa, hata katika uchache na udogo wao kama Jumuiya ya waamini. Kamwe wasikose kumwomba Yesu Kristo awaongezee imani.

Barua hii ya kichungaji imehaririwa na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.