2014-01-10 09:35:00

DRC ilifahamu kuhusu mashambulizi ya 30 Desemba 2013, lakini haikuyazuia!


Vikosi vya ulinzi na usalama vya DRC vilikuwa na taarifa ya njama ya mashambulizi, yaliyotokea tarehe 30 Desemba, 2013 huko Kinshasa, Lubumbashi, Kolwezi na Kindu lakini vilishindwa kuzuia mashambulizi haya kwa wakati. Hayo yamesemwa na Seneta Modeste Mutinga Mutuishayi mkurugenzi katika wizara ya mambo ya ndani ya nchi na vikosi vya ulinzi na usalama nchini DRC.

Wachunguzi wa mambo wanaendelea kujiuliza, ikiwa kama Vikosi vya Ulinzi na Usalama vilikuwa na taarifa ya mashambulizi haya, mbona havikutekeleza wajibu wake kiasi kwamba, watu wengi wakapoteza maisha na mali zao? Tarehe 30 Desemba, 2013, Kituo cha Televisheni cha Taifa, Makao makuu ya Vikosi vya Ulinzi na Usalama pamoja na uwanja wa Ndege wa N'djili vilishambuliwa na makundi ya watu waliokuwa na silaha kali.

Mashambulizi kama haya pia yalifanywa huko Lubumbashi na Kindu. Mashambulizi haya kadiri ya wachunguzi wa mambo yanaonekana kwamba, yalilenga zaidi kutaka kumkomboa Bwana Joseph Mukungubila Mutombo, aliyekuwa kati ya wagombea Urais nchini DRC kunako mwaka 2006.







All the contents on this site are copyrighted ©.