2014-01-09 09:29:57

Wacomboni wanavyochakarika kutoa huduma makini kwa waathirika wa ugonjwa wa Ukimwi, Nampula, nchini Msumbiji


Hospitali kuu ya Merrere mkoani Nampula, nchini Msumbiji kwa miaka mingi imekuwa mstari wa mbele katika huduma kwa wananchi wanaoishi katika makazi yasiyo rasmi ya Marrere. Wakati wa vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Msumbiji vilivyosababisha majanga na maafa makubwa, Hospitali hii ilikuwa imetelekezwa na Serikali. Ilianza kufanya kazi tena kunako mwaka 2005, baada ya Wizara ya Afya kutiliana mkataba na Jimbo kuu la Nampula, ili kukarabati na hatimaye kuiendesha.

Hospitali kuu ya Merrere inayoendeshwa na Shirika la Wamissionari wa Comboni, imekuwa ni kimbilio kubwa kwa wagonjwa na waathirika wa Ukimwi. Upendeleo wa pekee unatolewa kwa wanawake na watoto wenye virusi vya Ukimwi, ili kuwapatia dawa za kurefusha maisha sanjari na kukinga maambukizi mapya kutoka kwa Mama kwenda kwa mtoto.

Ni Hospitali inayotoa huduma za matibabu kwa waathirika pamoja na familia zao, ili waendelee kuishi kwa imani na matumaini, sanjari na kushiriki katika huduma kwa wale wanaowategemea. Wanawake wanafundishwa namna ya kuandaa lishe bora kwa watoto walioathirika kwa ugonjwa wa Ukimwi. Hospitali pia inatoa huduma kwa wagonjwa wanaoishi majumbani ambao hawana uwezo wa kufika Hospitalini hapo kupata tiba!







All the contents on this site are copyrighted ©.