2014-01-09 08:04:26

SIGNIS kufanya mkutano wake mkuu mjini Roma, Februari 2014


Mwaka 2013 umekuwa ni mwaka uliosheheni matukio makubwa ya kihistoria. Mwezi Machi Baba Mtakatifu Benedikto XVI akaamua kung’atuka kutoka madarakani kwa utashi wake kamili, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa la Kristo mchungaji mkuu. Makardinali wakamchagua Kardinali Jorge Mario Bergoglio kutoka Argentina kuliongoza Kanisa Katoliki kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Akachagua jina la Mtakatifu Francisko: fukara, mpenda amani na mtunza mazingira. RealAudioMP3

Tangu alipochaguliwa, Baba Mtakatifu Francisko ameonesha upendeleo wa pekee kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii si tu kwa maneno bali hata kwa mtindo wake wa maisha. Tarehe 17 Desemba, 2013, Kanisa linakungana na watu wenye mapenzi mema kuadhimisha kumbu kumbu ya miaka 77 tangu Baba Mtakatifu Francisko alipozaliwa.

Hivi ndivyo anavyoandika Bwana Augustine Loorthusamy, Rais wa Shirikisho la Vyama vya Mawasiliano ya Kanisa Katoliki Duniani, katika salam zake za Noeli ina Mwaka Mpya 2014. Anasema, Juni 2013, Sigins ilifuta mkutano mkuu wa Mwaka uliokuwa ufanyike mjini Beiruti, hapo Mwezi Oktoba, 2013 kutokana na vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria. Hali bado ni tete kwani kuna mateso na mahangaiko mengi ya watu wasiokuwa na hatia nchini Syria na Ukanda wa Mashariki katika ujumla wake.

SIGNIS baada ya tafakari ya kina, imeamua kufanya mkutano wake mjini Roma, hapo mwezi Februari 2014. Hii inatokana na ukweli kwamba, lisingekuwa ni jambo la busara kukaa na kuendelea kusubiria tena kwa kipindi cha miaka mingine minne bila ya kukutana. Uamuzi huu unazingatia changamoto mbali mbali zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu wa maendeleo ya sayansi na teknolojia ya habari. Mkutano huu utakuwa ni fursa ya kuchagua viongozi waandamizi wa SIGNIS pamoja na kuweka dira na mwongozo wa SIGNIS kwa miaka ijayo.

Rais wa SIGNIS anawaalika wajumbe kuhakikisha kwamba, wanashiriki kikamilifu katika maandalizi na hatimaye, Maadhimisho ya Mkutano mkuu hapo Mwezi Februari, 2014. Anawatakia wanachama wote kheri na baraka, amani na maendeleo kwa Noel ina Mwaka Mpya 2014.








All the contents on this site are copyrighted ©.