2014-01-08 09:38:04

Katiba nchini Tunisia kwa mara ya kwanza inaonesha usawa kati ya mwanaume na mwanamke mbele ya sheria


Kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi za Kiarabu, Bunge la Tunisia limepitisha mabadiliko ya kipengele cha Katiba kinachoruhusu usawa kati ya wanawake na wanaume nchini humo mbele ya sheria bila ubaguzi. Kipengele hiki kinazungumzia haki sawa miongoni mwa wananchi wa Tunisia.

Muafaka huu umefikiwa baada ya majadiliano ya kina yaliyofanyika kwa kipindi cha mwaka mmoja kwa kutaka yafanyike mabadiliko ya kipengele kilichokuwa kinaonesha ubaguzi wa kijinsi dhidi ya wanawake.

Mabadiliko haya yataanza kutumika, tarehe 14 Januari 2014, kama kielelezo cha kumbu kumbu ya kuanguka kwa utawala wa Zine El Abidine Ben Ali wa Tunisia, yapata miaka mitatu iliyopita. Huu ukawa ni mwanzo wa upepo wa mageuzi kwa nchi za Kiarabu! Katiba mpya inatoa haki kwa wananchi kutoa mawazo yao, kupata habari na kwamba, adhabu ya kifo imefutwa.

Baadhi ya vyama na mashirika ya kutetea haki msingi za binadamu yanasema kwamba, mabadiliko ya katiba bado yanayotoa mwanya wa wageni kutengwa nchini Tunisia, hata kama mabadiliko haya yanaonesha usawa kati ya mwanaume na mwanamke mbele ya sheria. Kanuni ya usawa bila ya ubaguzi inapaswa kuzingatiwa hata kwa wageni wanaoishi nchini Tunisia, vinginevyo, ubaguzi unaweza kujionesha kwa njia ya: rangi, dini na mwelekeo wa kisiasa anaofuata mtu!







All the contents on this site are copyrighted ©.