Idadi ya waamini na mahujaji waliokutana na Papa Francisko kwa Mwaka 2013 imeongezeka
maradufu!
Takwimu zinaonesha kwamba, tangu Baba Mtakatifu Francisko alipochaguliwa kuliongoza
Kanisa Katoliki hapo tarehe 13 Machi 2013, zaidi ya watu millioni sita wamekutana
na kushiriki katika matukio mbali mbali yaliyoendeshwa na Baba Mtakatifu katika kipindi
hiki hadi kufikia mwanzo mwa Januari 2014. Waamini, mahujaji na wageni walioshiriki
katika katekesi zake zinazotolewa kila Jumatano walikuwa ni1, 548, 500.
Baba
Mtakatifu alifanikiwa kukutana na kuzungumza na watu 87, 400 kwa faragha. Waamini
na mahujaji wapatao 2, 282, 000 walishiriki katika Ibada mbali mbali zilizoongozwa
na Baba Mtakatifu Francisko kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro na ndani
ya Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Waamini zaidi ya 2, 706, 000 wameshiriki
katika Sala ya Mchana na Baba Mtakatifu Francisko.
Takwimu hizi ni zile tu
zilizokusanywa mjini Vatican na wala hazihusishi matuko kama: Maadhimisho ya Siku
ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2013yaliyofanyika nchini Brazil, kule Rio de Janeiro;
wala safari zake za kichungaji ndani ya Italia, Lampedusa, Cagliari na Assisi hata
katika baadhi ya Parokia zilizoko katika Jimbo kuu la Roma.
Kwa ujumla waamini
na watu wenye mapenzi mema wapatao 6, 623, 000 wamekutana na kushiriki katika Ibada,
Katekesi na Sala zilizokuwa zinaongozwa na Baba Mtakatifu Francisko. Itakumbukwa kwamba,
idadi hii ya watu ni ile tu ambayo ni rasmi kwa wale watu walioomba tiketi kutoka
Vatican. Kumekuwepo na umati mkubwa wa watu wanaomiminika kwenye matukio mbali mbali
anayoshiriki Baba Mtakatifu Francisko, hii inatokana na mvuto alionao kwa watu!