2014-01-08 07:53:40

Chuo Kikuu cha SAUT


Ufunguzi wa Mwaka wa Masomo Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino cha Tanzania kwa Mwaka 2013-2014 lilikuwa ni tukio ambalo lilileta mvuto na mguso kwa wanafunzi wapya wanaoanza safari ya masomo yao Chuoni hapo. RealAudioMP3

Kila Mkuu wa kitivo, alipata nafasi ya kunadi na kuwatambulisha wadau mbali mbali watakaoshirikiana nao katika kunoa akili na kujipatia maarifa kutoka katika Chuo Kikuu cha SAUT, ambacho kwa sasa kinaendelea kupata mafanikio makubwa ndani na nje ya Tanzania.

Kwa ujumla wanafunzi walichangamotishwa na wakuu wa vitivo kuhakikisha kwamba, wanajenga utamaduni wa kujisomea ili kujifunza zaidi, huku wakizingatia rasilimali muda na kwamba, wapaswa kuonesha bidii na nidhamu ya kutaka kujipatia elimu, maarifa na ujuzi katika maisha yao Chuoni hapo.

Katika mchakato wa kujipatia elimu, watambue kwamba, kuna changamoto kubwa ambazo ziko mbele yao: hizi ni changamoto za ujana na uzee na kwamba, wanapaswa kujenga imani na matumaini kwa kile wanachokifanya. Chuo kikuu ni mahali ambapo wanapaswa pia kujifunza kuishi na wengine kama Jumuiya ya Wasomi, wakitambua kwamba, wanapaswa kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa SAUT. Umefika wakati kwa wanafunzi kuacha visingizio visivyo na tija wala mashiko kwa maisha yao kama wanafunzi. SAUT inaendelea kuboresha mitandao ya mawasiliano ili kuwapatia fursa ya kuweza kujifunza zaidi.

Hapa anasema Padre Thaddeus Mkamwa, Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha SAUT, taaluma kwamba, wanafunzi wanapaswa kujikita katika masomo na kuacha kupepeta mdomo! Waachane na matumizi mabaya ya mitandao na badala yake wajenge tabia ya kuwajibika zaidi wakitambua sadaka na majitoleo yanayofanywa na wadau mbali mbali katika mchakato wa kuhakikisha kwamba, wanapata elimu bora wawapo Chuoni hapo.

Vitivo mbali mbali vilivyoko SAUT vimepata mafanikio makubwa katika kipindi cha Mwaka wa Masomo 2012-2013. Haya ni mafanikio yaliyojionesha katika ngazi ya kitaifa na kimataifa. Kitivo cha sheria, mawasiliano ya jamii, elimu, biashara na uandisi ni kati ya vitivo ambavyo vinaendelea kufanya vyema zaidi. Kwa mfano kitivo cha sayansi ya mawasiliano ya Jamii, kimeendelea kuzalisha waandishi wa habari wanaotegemewa ndani na nje ya Tanzania kutokana na umakini, weledi, nidhamu na majitoleo yao wanapokuwa katika uwanja wa habari na mawasiliano. Hili ni jambo la kujivunia! Mafanikio kama haya yanajionesha pia katika kitivo cha elimu, ambacho ni kati ya vitivo vikongwe SAUT.

Wahadhili wa Chuo Kikuu cha SAUT wanaendelea kuhamasishwa kufanya tafiti na kuzichapisha kwa ajili ya mafao ya wasomi na Jamii kwa ujumla. Kitivo cha usimamizi wa biashara kimeendelea kuwaandaa wanafunzi kutoka SAUT katika ulimwengu wa kazi na ajira. Kinaendelea kuwekeza katika sekta ya utalii ili kuwajengea wanafunzi uwezo wa kutoa huduma bora, kwa kuimarisha utamaduni wa kushirikiana, kila mtu akijitahidi kutumia vyema karama na vipaji alivyokirimiwa na Roho Mtakatifu. Wanafunzi wa SAUT wanakumbushwa kwamba, hapo ni mahali pa kujenga na kuimarisha mapaji ya Roho Mtakatifu kwa ajili ya mafao ya wengi.

Kitivo cha uhandisi ni kati ya vitivo vichanga kabisa kwenye Chuo Kikuu cha SAUT, lakini kinapania kuhakikisha kwamba, kinachangia kwa kiasi kikubwa kuzalisha wahandisi watakaoshiriki katika kuleta ufumbuzi wa ukosefu wa wahandisi nchini Tanzania, jambo ambalo kwa sasa linaonekana kuwa kama “janga la kitaifa”. Takwimu zinaonesha kwamba, tangu Tanzania iliojipatia uhuru wake kutoka kwa Mwingereza kunako mwaka 1961 imefanikiwa kuandaa waandisi 13,000 tu.

Lengo la taifa lilikuwa ni kuwandaa wahandisi 80,000, jambo ambalo bado halijafikiwa. Wengi walioandaliwa wamekimbilia nje ya nchi ili kutafuta “malisho bora zaidi” na wachache waliopo wanaendelea kuzeeka na kung’atuka! Kitivo cha uandisi kitaendelea kuwekeza zaidi katika sekta hii kwani wahitimu wake wana uhakika wa kupata fursa za ajira. Hiki ni kitengo ambacho hakuna mgomo wa kazi, kumbe SAUT inaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa katika kukabiliana na “janga la ukosefu wa wahandisi Tanzania”

Kwa ufupi haya ndiyo yaliyojiri katika ufunguzi wa Mwaka wa Masomo, 2013-2014 Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino cha Tanzania, SAUT, hivi karibuni Jijini Mwanza. Tukio ambalo lilitanguliwa na Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Dr. Respicius Rugemalira, Mwanasheria mkuu wa SAUT na baadaye wakuu wa vitivo wakajinadi kwa sera, mikakati na matarajio yao kwa siku za usoni.

Kutoka SAUT, Jijini Mwanza ni
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.