Msipotoshe maneno ya Papa Francisko kuhusu ndoa za watu wa jinsia moja! Watoto wanahitaji
malezi ya Baba na Mama!
Padre Federico Lombardi msemaji mkuu wa Vatican anabainisha kwamba, kuna baadhi ya
vyombo vya habari nchini Italia vinavyopotosha kwa makusudi kuhusu maoni yaliyotolewa
na Baba Mtakatifu Francisko wakati alipokuwa anazungumza na viongozi wakuu wa Mashirika
ya Kitawa na Kazi za Kitume, hapo tarehe 29 Novemba 2013 kuhusu changamoto za malezi
kwa watoto na vijana wa kizazi kipya, tofauti kabisa na miaka kadhaa iliyopita!
Baba
Mtakatifu aliwaambia wakuu wa Mashirika kwamba, Familia nyingi kwa sasa zinakabiliana
na changamoto nyingi kwani: kuna wazazi waliotengana; kuna ndoa za watu wa jinsia
moja, mambo ambayo hayakuwepo kwa miaka kadhaa iliyopita. Elimu, malezi na urithishaji
wa imani hauna budi kuzingatia changamoto hizi kwa ajili ya mafao ya vijana wa kizazi
kipya; wanaopaswa kusindikizwa kwa busara ya hali ya juu mintarafu hali na mazingira
ya familia wanamotoka, ili hata wao, waweze kupokea zawadi ya imani katika mwelekeo
chanya!
Padre Federico Lombardi anasema, maoni haya ya Baba Mtakatifu yanagusia
dhamana na utume wa Kanisa katika masuala ya elimu na malezi katika ujumla wake na
wala si mwelekeo wa Baba Mtakatifu Francisko wa kutaka "kupigia debe" ndoa za watu
wa jinsia moja kama ambavyo baadhi ya vyombo vya habari nchini Italia vinavyotaka
kuwasadikisha watu.
Baba Mtakatifu alitolea mfano wa mtoto ambaye alijikuta
akiwa ameelemewa na huzuni kutokana na ukweli kwamba, mchumba wa mama yake alikuwa
hampendi. Haya ndiyo mateso na mahangaiko wanayokabiliana nayo watoto katika maisha
ya ndoa na familia. Waamini na watu wenye mapenzi mema, wawe makini kwani kuna watu
kwa makusudi mazima wanataka kupotosha ukweli kwa ajili ya mafao yao binafsi. Watoto
wanahitaji malezi ya baba na mama kadiri ya mpango wa Mungu katika maisha na mwanadamu!