2014-01-07 10:41:12

Matumaini ya kupata chanjo dhidi ya Malaria kwa Mwaka 2014?


Kuna matumaini makubwa kwa Bara la Afrika katika kipindi cha Mwaka 2014 kuweza kupata kinga dhidi ya ugonjwa wa Malaria ambao umekuwa ni tishio kwa maisha na maendeleo ya wananchi wengi Barani Afrika. Majaribio ya chanjo yaliyofanywa kwa watoto 15, 500 yanaonesha kwamba, ugonjwa wa Malaria ulipingua kwa kipindi cha miezi 18 ya majaribio ya chanjo hii mpya.

Kampuni ya GlaxosmithKline inatarajiwa kuwasilisha chanjo hii kwa Taasisi ya Ulaya kwa uchunguzi wa kina kabla ya kuanza kuuzwa madukani. Chanjo hii inaonesha mafanikio ingawa bado kuna mashaka kidogo yanayofanyiwa kazi na wataalam wa chanjo. Takwimu za Shirika la Afya duniani zinaonesha kwamba, kwa Mwaka 2010 watu waliofariki dunia kutokana na ugonjwa wa Malaria walikuwa ni 666, 000 na zaidi ya watu millioni tatu walishambuliwa kwa ugonjwa wa Malaria duniani, hali ambayo inatishia usalama wa maisha ya watu wengi duniani.

Waathirika wakubwa wa ugonjwa wa Malaria ni watu wanaoishi Kusini mwa Jangwa la Sahara na Asia. Dawa nyingi zinazotumika dhidi ya ugonjwa wa Malaria zimewafanya watu wengi kuwa sugu, jambo ambalo linahatarisha usalama wa maisha ya watumiaji wa dawa hizi. Usafi wa mazingira pamoja na utumiaji wa vyandarua vyenye dawa ni jambo muhimu sana katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Malaria duniani.

Upatikanaji wa chanzo ya ugonjwa wa Malari ni jambo la kutia matumaini kwa watu wengi wanaoteseka kutokana na ugonjwa huu sehemu mbali mbali za dunia. Wataalam wanasema, si jambo rahisi kupata chanjo dhidi ya ugonjwa wa Malaria ambao umekuwa sugu kwa miaka mingi. Chanjo inayofanyiwa majaribio ni changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa katika mchakato wa kutaka kudhibiti ugonjwa wa Malaria duniani.







All the contents on this site are copyrighted ©.