Anzeni Mwaka Mpya wa 2014 kwa kuwa na maisha mapya yanayosimikwa katika misingi ya
imani, matumaini na mapendo!
Baraza la Maaskofu Katoliki Ufilippine katika salam zake za Mwaka Mpya wa 2014, linawaalika
waamini kutubu na kuongoka, ili kuachana na maisha ya zamani, tayari kuuanza Mwaka
Mpya kwa maisha yanayosimikwa katika imani, matumaini na mapendo; fadhila ambazo zinapaswa
kujionesha katika uhalisia wa maisha ya kila siku.
Askofu mkuu
Socrates Villegas wa Jimbo kuu la Lingayen- Dagupan ambaye pia ni Rais wa Baraza la
Maaskofu Katoliki Ufilippini anasema, kuna haja kwa waamini na watu wote wenye mapenzi
mema kujikita katika toba na wongofu wa ndani, ili kuuvua utu wa kale uliochakaa kutokana
na rushwa pamoja na uvunjifu wa misingi ya haki, amani na utulivu.
Umefika
wakati kwa wananchi wa Ufilippini kuondokana na tabia ya kuteka watu nyara, kujikita
katika vitendo vya kigaidi na rushwa; mambo ambayo kimsingi yanahatarisha amani, ustawi
na maendeleo ya wananchi wa Ufilippini ambao kwa sasa wanakabiliana na changamoto
nyingi za maisha!
Askofu mkuu Villegas anawatakia waamini na watu wote wenye
mapenzi mema, Mwaka Mpya wa 2014, ili uwe ni mwanzo wa maisha mapya yanayosimikwa
katika haki, amani, upendo na upatanisho wa kitaifa. Kanisa nchini Ufilippini linasali
kwa ajili ya kuombea amani nchini Syria, ili wananchi waweze kupata ujasiri wa kujipatanisha
na Mungu pamoja na ndugu zao. Wanasali na kuwaombea wananchi wa Ufilippini walioathirika
na tufani iliyotokea hivi karibuni nchini mwao, ili waweze kupiga moyo konde na kupata
ujasiri wa kuanza upya tena, kuchakarika ili kujiletea maendeleo zaidi.
Mwaka
Mpya ni Siku ya Kuombea Amani Duniani. Ni Siku ya kuombea mshikamano wa kimataifa
dhidi ya baa la njaa, ujinga na umaskini sehemu mbali mbali duniani. Ni muda wa kusali
na kuombea amani, utulivu na maendeleo ya wengi, huku watu wakijitahidi kukumbatia
huruma na upendo wa Mungu unaojionesha kwa njia ya Yesu Kristo aliyemwaga damu yake
azizi kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu.
Baraza la Maaskofu Katoliki Ufilippini
linawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuanza Mwaka Mpya wa 2014 kwa
imani, matumaini na mapendo kwa Mungu na Jirani. Watu wamtangulize Mungu katika maisha
na mipango yao, ili waweze kuonja upendo na huruma kwa waja wake. Waamini wasisite
kukimbilia ulinzi na tunza ya Bikira Maria Mama wa Mungu.
Waamini wasimame
kidete kulinda, kutetea na kushuhudia Injili ya Uhai, dhidi ya utamaduni wa kifo,
kama njia ya kumuenzi Bikira Maria aliyekubali kuwa ni Tabernakulo ya kwanza ya Neno
wa Mungu aliyefanyika Mwili, akawa mwanadamu katika mambo yote isipokuwa hakutenda
dhambi. Yesu ni Mungu kweli na mtu kweli! Huu ni mwaliko kwa kila mwamini pia kutengeneza
mazingira katika maisha yake, ili Yesu aweze kupata makao ya kudumu; daima wakiwa
tayari kumsikiliza na kutii amri na maagizo yake.