2014-01-06 15:56:37

Papa atangaza hija yake katika Nchi Takatifu


Papa Francisko, Jumapili, alitangaza kwamba ana mpango wa kufanya hija Nchi Takatifu mwezi Mei mwaka huu. Tamko hili amelitoa ikiwa imepita siku moja tu, baada ya kupita kumbukumbu ya miaka 50, tangu Khalifa wa mtume Petro , Papa Paulo VI, kufanya ziara ya kihistoria ya kwanza , nje ya Italia, kutembelea maeneo Matakatifu mjini Bethlehemu , Yerusalemu na Nazareth - Januari 4, 1964.
Ziara hii ya kwanza nje ya Italia ya Papa Paulo VI, ilifungulia mlango wa safari zingine, hatimaye kutembelea mabara sita, ikiandika pia historia ya kwanza ya Mkuu wa Kanisa la Ulimwengu , Baba Mtakatifu na Askofu wa Roma, kutumia usafiri wa ndege kwa mara ya kwanza. Historia inaonyesha Hija hiyo ya kwanza ya Papa Paulo VI, pia iliweka alama ya mabadiliko ya msingi katika mahusiano kati ya Kanisa Katoliki na Kanisa la Ki-Orthodosi ambamo Papa Paul VI alikutana na mkuu wa Kanisa la Kiothodosi wakati huo, Patriaki wa Kiekumeni wa Constantinople, Mwenye Heri Athenagoras I, katika bustani ya Mizeituni ya Yerusalemu . Kukutana kwao kuliweza kuondoa vikwazo vilivyo kuwepo, kwa pande zote mbili, baada ya utengano wa Makanisa ya Mashariki na Magharibi, tangu upinzani wa mwaka 1054.
Papa Fransciko Jumapili akizungumza na mahujaji waliojitosa katika hali mbaya ya hewa na kwenda kusali pamoja nae sala ya Malaika wa Bwana na kumsikiliza , alisema , katika furaha ya msimu huu wa noel, napenda kutangaza kwamba kuanzia Mei 24-26 ijayo , Mungu akipenda, nitafanya hija katika Nchi Takatifu.
Baba Mtakatifu alitaja lengo kuu la hija hii yake, ni kushiriki katika kumbukumbu ya kutimia miaka 50 tangu Papa Papa Paulo VI na Patriaki Athenagoras , walipokutana mnamo Januari 5, 1964. Na kwamba, anapanga kutembelea miji ya Amman, Bethlehemu na Yerusalemu. Pia kwamba alipenda kushiriki katika Mkutano wa kiekumeni , utakao fanyika katika Kanisa la Kaburi Takatifu na hudhuriwa na wawakilishi wa Makanisa ya Kikristo ya Yerusalemu , pamoja na Patriaki Bartholomew I wa Constantinople.
Papa alimalizia ujumbe huo kwa kuomba sala za waaamini zimsindikize katika nia na Hija hii."

Jumapili hiyo, Kabla ya Sala ya Malaika wa Bwana, Papa Francisko alielezea jinsi sherehe za Noel, zinavyonyesha upendo mkubwa Mungu alio nao kwa binadamu. Na kwamba kila adhimisho la kuzaliwa kwa Yesu duniani ni adhimisho jipya, kwa ajili ya dunia kufanywa upya. Mungu , alisema, daima yupo tayari kuwalea waume kwa wake, na kuutakatifu ulimwengu dhii ya dhambi , na Yesu daima hachoki kuwa nasi na hakomi kutujalia neema yake ya kuokoa. Papa alikamilisha hotuba yake kwa kuwashukuru wote waliomtumia salaam za matashi mema wakati wa Noel na mwaka mpya, na kwa moyo wao wa kufiki kumsikiliza licha ya hali mbaya ya hewa.

Ziara ya Papa Paulo VI, kutembelea Nchi Takatifu 1964, ilifuatiwa na ziara ya Papa Yohane Paul II, wakati wa Jubilee mwaka 2000. Ziara hii ilichukuliwa katika mitazamo yote miwili, kama binafsi, na pia kuwa hija ya kiroho katika eneo lenye mizizi ya imani ya Kikristu , na pia kama ziara ya kidiplomasia iliyolenga kuimarisha maridhiano kati ya Wakristo, Waislamu na Wayahudi wanaoishi Mashariki ya Kati.

Katika ziara hiyo , kati ya picha za kukumbukwa, ni wakati ambapo Papa Yohane Paul II, alipotolea sala zake katika jadi ya kiyahudi ya kuomboleza katika ukuta wa Yerusalem na kuacha karatasi ya sala katika moja ya nyufa za ukuta huo. Iliwashangaza wengi kwamba, Papa Yohane Paulo katika karatasi ya sala hiyo, aliomba msamaha wa Mungu kwa ajili ya dhambi za Wakaristu dhidi ya Wayahudi.

Papa Benedict XVI nae alifuata nyayo za watangulizi wake, na kutembelea Yerusalemu Mei 2009. Na kati ya maeneo mengine aliyozuru ni Mnara wa kumbukumbu ya mauaji wa kinyama dhdi ya wayahudi, mnara wa Yad Vashem, Ambako pia alikutana na waathirika wamadhulumu ya kinyama yaliyofanywa na maaskari wa Nazi. Papa Benedikto XVI, mahali hapo alitoa wito na ahadi ya Kanisa kusaidia kuhakikisha kwamba, chuki dhidi ya Wayahudi, kamwe isiruhusiwe kuwepo tena duniani.








All the contents on this site are copyrighted ©.