Miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar: baadhi ya mafanikio!
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete ameisifu Zanzibar kuwa
ni nyota inayong’ara ya mapambano dhidi ya ugonjwa wa malaria katika Afrika akisisitiza
kuwa siyo tu kwamba, inaongoza katika Afrika lakini ni mfano wa kuigwa duniani. Aidha,
Rais Kikwete ameisifu na kuipongeza Zanzibar kwa kuvuka lengo la Shirika la Afya Duniani
(WHO) la kuhakikisha kuwa wananchi hawatembei umbali wa zaidi ya kilomita tano kufuata
huduma ya afya. Zanzibar imeshuka kutoka umbali wa kilomita tano kama inavyopendekezwa
na WHO hadi kufikia kilomita tatu.
Rais Kikwete pia amekisifu Kikosi Maalum
cha Kupambana na Magendo (KMKM) cha Zanzibar kwa kazi nzuri ya kulinda mipaka ya majini
na kudumisha utulivu ambao Tanzania imeushuhudia katika miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar
ambayo kilele cha sherehe zake kitakuwa Jumapili ya Januari 12, mwaka huu, 2013.
Rais
Kikwete amezungumza hayo Jumamosi, Januari 4, 2014, na mamia ya wananchi, maofisa
na askari wa KMKM baada ya kuifungua rasmi hospitali kubwa na ya kisasa ya Kikosi
hicho kwenye eneo la Kibweni mjini Zanzibar. Rais Kikwete ambaye yuko katika ziara
ya siku mbili ya kikazi katika Zanzibar amefungua rasmi hospitali hiyo ikiwa ni sehemu
ya shamrashamra za Sherehe ya Miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Akizungumzia
mafanikio ya Serikali ya Mapinduzi (SMZ) katika miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar
katika nyanja mbali mbali, Rais Kikwete amesema kuwa Zanzibar imekuwa na mafanikio
makubwa na ya kujivunia katika kipindi hicho. Rais amesema kuwa moja ya mafanikio
makubwa yamekuwa katika sekta ya afya ambako miongoni mwa mambo mengine Zanzibar imefanikiwa
kufuta ugonjwa wa malaria Visiwani. “Haijawahi kutokea katika Afrika nchi yoyote ikafanikiwa
kutokomeza ugonjwa wa malaria. Hapa Zanzibar imewezekana na kwa kweli kama siyo mlolongo
wa masharti ya kimataifa, Zanzibar ingeweza tayari kutangaza kuwa Zanzibar imefuta
malaria.”
Rais Kikwete alikuwa anazungumzia takwimu za Waziri wa Afya wa Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mheshimiwa Juma Duni Haji ambaye alikuwa amemwambia Rais
Kikwete kuwa mwaka 2007, vifo vilivyotokana na ugonjwa wa malaria vilikuwa asilimia
3.1 lakini mwaka 2011 asilimia hiyo ilikuwa imeshuka hadi sifuri.
Mheshimiwa
Haji amesema kuwa mwaka 2004/5, uwepo wa ugonjwa wa malaria katika Zanzibar ulikuwa
asilimia 44.6 lakini mwaka juzi, 2012, asilimia hiyo ilikuwa imeshuka na kuwa chini
ya asilimia moja. Kutokana na takwimu hizo, Rais Kikwete amesema: “Mafanikio ya Zanzibar
katika kukabiliana na malaria hayajawahi kufikiwa na nchi yoyote katika Afrika. Zanzibar
ni nyota inayong’ara katika kukabiliana na ugonjwa wa malaria.”
Hata hivyo,
Rais Kikwete ameonya kuwa ni muhimu kwa Zanzibar kuendelea kudumisha hatua zote ambazo
zimeleta mafanikio hayo vinginevyo “tutarudi nyuma kama ilivyopata kutokea huko tulikotoka.
Hii ni mara ya tatu kwa Zanzibar kufikia hatua nzuri kiasi hiki. Nataka tudumishe
hali hii iwe ya kudumu siyo kurudi nyuma kama iliyopata kutokea mara mbili nyuma.”
Kuhusu
mafanikio ya Zanzibar ya kupunguza masafa ya wananchi wake kupata huduma angalau kufikia
kilomita tatu, Mheshimiwa Haji amesema: “Kwa furaha kubwa, naomba kukueleza wewe Mheshimiwa
Rais pamoja na wageni wetu kuwa Zanzibar imefanikiwa kufikia lengo hili kwa muda mrefu
sasa na kulipindukia. Hakuna mwananchi wa Zanzibar anayesafiri zaidi ya kilomita tatu
kutoka kituo kimoja cha afya kwenda kingine.”
Rais Kikwete amepongeza hatua
hiyo akisisitiza kuwa mafanikio hayo katika afya kama ilivyo katika sekta nyingine
ni ushahidi usiopingika wa usahihi wa Mapinduzi ya Januari 12, mwaka 1964, kwa sababu
mapinduzi yalikuwa na shahaba ya kuleta maendeleo kwa kuwaondoa wale ambao walikuwa
hawatafuti maendeleo ya wananchi wa Zanzibar.