2014-01-06 15:43:06

Mamajusi hutufundisha kuitetea imani dhidi ya ujanja wa uovu.


Tukio la Mamajusi kwenda kumwona Mtoto Yesu pangoni, hufundisha jinsi ya kuweka imani dhidi ya ujanja na ulaghai wa kutumia mambo matakatifu kutenda maovu. Papa alieleza katika homilia yake, wakati wa Ibada ya Misa aliyoiongoza katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro, Asubuhi ya Jumatatu, kwa ajili ya maadhimisho ya Siku Kuu ya Epifania. Siku Kuu ya Kumtolea Bwana shukurani na zawadi, kama walivyofanya watalaam wa nyota, kwenda kumwabudu mtoto Yesu pangoni Bethlehemu, wakiwa wamechukua zawadi zao mbalimbali .
Papa alionya dhidi ya kumtafuta Mungu kwa imani nusunusu, wasiwasi na hofu na ulaghai wa kutaka kufanikisha maovu. Papa alitoa wito kwa waamini, wawe macho kuungudua ujanja unaoweza kutumiwa na roho ya mwovu, katika kufanikisha malengo yake kama alivyofanya Herode wakati alipokutana na wataalamu wa nyota, na kuwaambia “nendeni mkapate habari za Mtoto Yesu ili nami niende kumwabudu”. Papa aliendeela kufafanua kwamba, Tukio la Epifania ni kuufuata mwanga kwa uvumilivu mpaka kuungudua mahali ulipo mwanga mkubwa, wenye kuleta mabadiliko kwa ajili ya maisha ya milele. Siku Kuu ya Epifania, ni sawa na kutembea katika hali ya unyonge katika giza linalo mulikiwa na nuru ndogo lakini kali, pia linatuonyesha jinsi za ulaghai wa wasio aminifu, wanavyo fanya njama za kulinda marupurupu yao. Papa Francisko, alieleza na kuzitaja alama za Nyota, mamajuzi na Herode, akisema zinaonyesha hatua kuu katika kuitafuta Nuru, Yesu Kristo.

Watalaam wa nyota, kwa uaminifu waliifuta nyota iliyowaongoza hadi kukutana na Bwana. Safari hii ya wataalamu wa nyota wa Mashariki, kwetu sisi inakuwa ni mfano wa hatima ya kila mmoja wetu, katika safari yake maisha , inayoonyesha kwamba, maisha yetu ni kutembea katika barabara inayo angaziwa na mwanga wa kuupata ukamilifu wa ukweli na upendo, kwa sisi Wakristo, tunatambua mwanga huo kuwa ni Yesu, Nuru ya ulimwengu.

Wakristo wa leo, Papa alibainisha, wana nyota yao, nayo ni Injili ya Kristu , ambayo huisoma na kuitafakari kila siku kwa ajili ya kuishi na Yesu na upendo wake. Lakini katika njia hii ya kuifuata nuru hiyo, inaweza kutokea muumini kuipoteza kidogo nuru ya nyota kama ilivyotokea kwa Mamajusi , hata kuangukia katika uvuli wa Herode, aliyejawa na wasiwasi na mashaka juu ya kuzaliwa kwa mtoto mdogo , katika hali ya unyonge, lakini aliyemshakia kuwa ni Mkuu kuliko yeye Herode.. Lakini Yesu hakuja kumpindua Herode wala kuwa mfalme wa dunia hii, hivyo Herodi aliingiwa na wasiwasi wa bure, aliingiwa na hofu hadi yeye na washauri wake wakatoa sheria ya kuua watoto wote wa kiume. Sheria ya mauaji ya watoto. Ni hofu gani hii! Papa alieleza na kuonya dhIdi ya muumini kuwa na wasiwasi wa aina hii ambao unaweza si kuua watoto kimwili tu lakini pia unaoweza kusababisha hata mauaji ya kiroho . Ni hofu, yenye kutia wendawazimu .
Papa alimalizia homilia akisema yote haya yanatupa fundisho la kutokuwa waamini nusunusu, waliojaa wasiwasi na mashaka badala ya kwa na imani imara, yenye kuvutia katika maisha makamilifu ya wema na ukweli. Na pia tunapata fundisho kwamba tusikubali kudaganywa na mambo makuu ya kidunia au kudaganywa na wenye mamlaka , lakini la muhimu zaidi ni kuilinda imani yetu na kuitetea daima. Ni kwenda Bethlehemu , katika nyumba ya kawaida, nje ya mji, ambako kuna mama na baba waliojawa na upendo na imani , wenye kuutazama Mwanga wa Jua kutoka juu , ambaye ndiye Mfalme wa ulimwengu.








All the contents on this site are copyrighted ©.